Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya viongozi kadhaa wa upinzani waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi ya rais jijini Nairobi.
Viongozi hao walioandamana na kundi dogo la raia walitaka kuwasilisha barua kwa rais kuorodhesha matakwa yao japo mpango wao ulitibuka walipoagizwa kuondoka mara moja na kufyatuliwa mabomu.
Ripoti katika mitandao ya kijamii imeonesha watu wachache wakikimbizana na polisi katika baadhi ya maeneo, tofauti na hali ilivyokuwa katika maandmano ya wiki chache zilizopita ambapo maelfu ya watu walishiriki maandamano ndani na nje ya jiji la Nairobi.
Pia baadhi ya picha zilizosambazwa mtandaoni zimeonesha basi moja limechomwa moto pamoja na gari ya mizigo, huku baadhi ya viongozi serikali wakidai kuwa wahusika ni waandamanji kutoka upinzani. Hata hivyo upande wa upinzani umekanusha madai hayo.
Taswira mjini
Barabara nyingi katikati mwa jiji la Nairobi zimesalia kimya huku maduka yakifungwa kwa kuhofia uharibifu wa mali, hali iliyojitokeza katika maandamano yaliyofanyika awali.
Watu wachache walijitokeza katika maeneo kadhaa tu kushiriki maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa chama cha Azimio, Raila Odinga, akitaka rais kuwajibikia hali ngumu ya maisha nchini Kenya.
Magari ya polisi yametumika kufunga barabara kuu za kuelekea katikati mwa jiji, huku mamia ya polisi wa kukabiliana na ghasia wakishika doria.
Matakwa ya Raila
- Kufanywa uchunguzi wa kina kwa mashine za kurekodi matokeo ya uchaguzi ya mwaka wa 2022
- Kubatilishwa uteuzi na kuajiriwa kwa maafisa wa tume ya uchaguzi, IEBC, nchini
- Kufanyia ugatuzi shughuli za tume ya uchaguzi na kutoa nguvu huru kwa vyombo husika katika uchaguzi
- Kuweka misingi bora ya kufanywa uchaguzi huru na wa haki yenye matokeo ya wazi
-Kupunguza gharama yamaisha ikiwemo kupunguzwa kwa bei za mafuta, unga na mgao wa umeme nchini
Mazungumzo
Mnamo mwezi Aprili, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alitangaza kusitisha maandamano, kwa kuitikia wito wa rais William Ruto wa kufanya mashauriano kwa njia ya amani.
Hata hivyo baada ya kukutana kwa siku chache tu pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana juu ya wawakilishi katika mazungumzo hayo huku wote wakishutumiana kwa kukosa uaminifu na uwazi katika mazungumzo hayo.
Azimio iliwatangazia wafuasi wake kuwa, wana nia ya kundelea na maandamano huku mashauriano yakifanyika kama njia ya kushinikiza serikali kuwajibikia upande wake.
Polisi nao wamesisitiza kuwa maandamano hayo hayafuati utaratibu wa sheria nchini.