Jaji Kathurima Minoti, Agnes Murgor, na John Mativo walisema hivyo leo tarehe 31 Julai .
Majaji walisema kuwa mchakato uliopelekea kutungwa kwa Sheria ya Fedha ya 2023 ulikuwa na dosari kubwa na ulikiuka katiba na kwamba hauwezi tumika sasa.
"Hivyo basi, tunatoa tangazo hili kwamba kutungwa kwa Sheria ya Fedha ya 2023 kulikiuka Kifungu cha 220 (1) (a) na 221 cha katiba kama ilivyosomwa pamoja na vifungu vya 37, 39 na 40 vya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMA) ambayo inaelekeza mchakato wa kutengeneza bajeti, hivyo kufanya Sheria inayofuatia ya Fedha, 2023 kuwa na dosari kubwa na hivyo ni kinyume cha katiba."
Serikali ya Kenya itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, afisa wa ngazi ya juu serikalini aliiambia TRT Afrika siku ya Jumatano.
Serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo
"Tamko la mahakama lina athari kubwa. Ni nini kitakachotokea kwa fedha zilizokusanywa tayari? Nafikiri kuna upindukaji wa mamlaka ya mahakama nchini Kenya. Kama serikali, bila shaka tutapinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika Mahakama ya Juu," afisa wa serikali, ambaye alizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema.
Kenya ilikuwa imetayarisha bajeti ya shilingi trilioni 3.7 ($28.5 bilioni) kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Hivi karibuni serikali ililazimika kurudi kutumia bajeti hiyo baada ya Rais Ruto kukataa kusaini Muswada wa Fedha wa 2024 kuwa sheria kufuatia maandamano ya siku kadhaa nchini.
Iwapo serikali itashindwa kukata rufaa katika Mahakama ya Juu, italazimika kuendana na matumizi ya Sheria ya Fedha ya 2022.