Palestina yawasilisha ombi la kuiongezea nguvu kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli

Palestina yawasilisha ombi la kuiongezea nguvu kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli

Hadi kufikia sasa, nchi tisa zimeshapeleka maombi ya aina hiyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
Athari za mashambulizi ya majeshi ya Israeli katika eneo la Gaza./Picha: Reuters

Palestina imesema kuwa imepeleka ombi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuiunga mkono Afrika Kusini katika kesi yake dhidi ya Israeli.

Palestina iliwasilisha "ombi la ruhusa ya kuingilia kati kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli kuhusu Utumizi wa Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari katika Ukanda wa Gaza" katika ofisi ya usajili ya mahakama mnamo Mei 31, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Palestina WAFA.

Pia, iliyataka mataifa yote ambayo yameridhia Mkataba wa Mauaji ya Kimbari "kujiunga na taratibu za kesi zilizowasilishwa na Afrika Kusini, kuwalinda watu wa Palestina kutokana na uhalifu wa mauaji ya kimbari, kuhakikisha kutorudiwa kwa uhalifu huu mbaya katika siku zijazo.

Hivi karibuni, Chile ilijiunga katika kesi kama ilivyotangazwa na Rais Gabriel Boric, siku ya Jumamosi.

Hadi kufikia sasa, nchi tisa zimeshapeleka maombi ya aina hiyo au kuonesha nia hiyo, zikiwemo Nicaragua, Colombia, Libya and Mexico.

Mwanzoni mwa mwezi Mei, Uturuki ilisema kuwa itawasilisha rasmi ombi la kuwa sehemu ya kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli katika Mahakama ya ICJ, kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan.

Israeli imeendelea na mashambulizi yake dhidi ya Gaza tangu kutokea kwa shambulio la mpakani la Hamas, Oktoba 7 mwaka jana.

Zaidi ya Wapalestina 36,400 wameuwawa tangu kutokea kwa mashambulizi hayo, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, huku zaidi ya watu 82,600 wakijeruhiwa, kulingana na mamlaka za ndani za afya.

Miezi nane tangu kutokea kwa mashambulizi hayo, maeneo mengi ya Gaza yamegeuka kuwa magofu huku kukiwa na vizuizi kwenye upatikanaji wa chakula, maji safi na dawa.

Israeli inashutumiwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo katika hukumu yake ya hivi karibuni iliitaka kusitisha mashambulizi yake katika eneo la kusini la Rafah.

TRT Afrika
AA