Na Charles Mgbolu
Waandaaji wa Tuzo za 96 za Academy (Oscars 2024) wametangaza orodha yao ya wateule, huku filamu ya Marekani ya maisha ya mwanasayansi "Oppenheimer" ikipata uteuzi mwingi zaidi.
Filamu hiyo ya kutisha ilipata uteuzi 13, ikifuatiwa na filamu ya vichekesho vya kisayansi "Poor Things," ambayo ilipata uteuzi 11.
Watengenezaji filamu kutoka bara la Afrika pia wamepata nafasi za kazi zao kuteuliwa katika vipengele mbalimbali.
Filamu ya kumbukumbu ya Uganda ‘Bobi Wine: The People's President’ iliyoandikwa na kuongozwa na Christopher Sharp na Moses Bwayo iliteuliwa katika kipengele cha Best Documentary Feature au filamu inayoonesha hali halisi.
Filamu hiyo, inayohusu maisha na matarajio ya mwanamuziki wa Uganda aliyebadilika kuwa mwanasiasa Bobi Wine, ilizinduliwa katika toleo la 79 la Tamasha la Filamu la Venice.
"Ni wakati wa unyenyekevu kuona hadithi ya Uganda ikifika kwenye Tuzo za Academy, tuzo zenye heshima na umuhimu mkubwa zaidi ulimwenguni... Asante kwa utambuzi huu!" Bobi Wine alisema kwenye X.
"Four Daughters," filamu ya Tunisia, pia iliteuliwa katika kipengele cha Best Documentary Feature.
Iliandikwa na kuongozwa na Kaouther Ben Hania na inasimulia hadithi ya mama wa Tunisia anayetafuta kwa udi na uvumba binti zake wawili walio potea.
Filamu hiyo ilishindania Tuzo ya Palme d'Or katika Tamasha la 76 la Filamu la Cannes, ambapo ilikuwa na uzinduzi wake wa kimataifa tarehe 19 Mei, 2023.
Iliteuliwa kama filamu ya Tunisia kwa ajili ya Tuzo ya Best International Feature Film katika Tuzo za 96 za Academy na iliteuliwa kwa Best Documentary Feature.
Filamu ya Senegal ‘Io Capitano’ ni filamu ya tatu iliyoteuliwa kwa Oscars za mwaka huu.
"Lo Capitano" inaelezea safari ya kusisimua ya wavulana wawili wadogo, Seydou na Moussa, ambao wanapaswa kupambana na changamoto mbalimbali wanaposafiri kutoka Dakar kwenda Ulaya.
Filamu hiyo iliandikwa na kuongozwa na mtengenezaji filamu wa Italia, Matteo Garrone, na ilishindana katika Tamasha la 80 la Kimataifa la Filamu la Venice, ambapo ilishinda tuzo ya Simba wa Fedha.
Pia iliteuliwa kwa Best Foreign Language Film - filamu ya lugha za nje katika Tuzo za 81 za Golden Globe na Best International Feature Film, filamu bora ya kimataifa, katika Tuzo za 96 za Academy.
Tuzo za 96 za Academy zitafanyika katika sherehe ya kifahari huko Los Angeles, Marekani, tarehe 10 Machi.