Na Hamza Kyeyune
Kama siku ipambazukayo, ndivyo bara la Afrika linavyopambana na changamoto za ongezeko la idadi ya vijana, kuongezeka kwa umri wa kuishi, hali inayotokana na maendeleo katika sayansi, lishe na afya ya umma.
Hata hivyo, Afrika bado inakumbana na changamoto kubwa kwenye eneo la hifadhi ya jamii, ikiwa ni pamoja wastaafu kushindwa kujikimu kimaisha.
Baadhi ya wataalamu, wameonesha wasiwasi wao wa wazi, wakisisitiza kwamba suala hili linabakia kuwa la dharura, hasa ukitilia maanani vipaumbele vingine katika maisha, kama vile afya, elimu, maendeleo ya kilimo na usalama.
Kwa mujibu wa Shirika linalohudumia Wazee Duniani (Help Age International) watu wenye umri zaidi ya miaka 60 na 80, wanawakilisha kundi la watu linalokuwa kwa kasi zaidi katika bara la Afrika.
Wakati idadi ya wazee ikiongezeka kwa asilimia 50, kati ya mwaka 2000 na 2015, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kufikia 2050, dunia itakuwa mwenyeji wa watu takribani bilioni mbili, wenye miaka zaidi ya 60 duniani kote, ambapo karibu asilimia 80 ya watu hao, wataishi katika nchi zinazoendelea.
Kuziba Mashimo
Wakati Afrika iko katika hatua ya mabadiliko ya kidemografia katika historia yake, nchi nyingi ndani ya bara hilo linakosa mifumo bora ya pensheni na hifadhi ya jamii ya umma.
Kulingana na utafiti unaojulikana kama "Mifumo ya Kimataifa ya Utoaji wa Pensheni", na kuandaliwa kwa pamoja na Robert Palacios na Montserrat Pallarès-Miralles, chini ya asilimia 10 ya idadi ya wazee kusini mwa jangwa la Sahara, wanapata mafao yao kwa njia ya kuchangia.
Hata takwimu zilizowasilishwa na wajumbe katika mkutano wa nne wa mwaka wa Chama cha Wasimamizi wa Pensheni wa Afrika (APSA) mjini Kampala Novemba mwaka jana zilionyesha uzito wa tatizo hilo.
Wajumbe wa mkutano huo uliokuwa na mada "Mafao Shirikishi na Endelevu Afrika", walibainisha kuwa watu milioni 600 kati ya milioni 778 wenye umri wa kufanya kazi barani Afrika hawapati mafao yao kutoka mashirika ya hifadhi za jamii. Ukweli huu unatoa taswira kwamba watu hao wana hatari ya kuishi katika dimbwi la umasikini, baada ya kustaafu.
Mfano wa Uganda
Uganda, ambayo pia ni mwanachama wa APSA, ina waokoaji milioni tatu waliosajiliwa, ambayo ni sawa na idadi ya watu wanaofanya kazi ya zaidi ya watu milioni ishirini.
Kulingana na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Mafao ya Kustaafu ya Uganda (URBRA), Martin Nsubuga, ukosefu mkubwa wa ajira na viwango vya umaskini, ukosefu wa usawa kidijitali, utumaji michango isivyo kawaida , na akiba isiyotosheleza ndizo sababu zinazowatenga Waganda wengi na mifuko ya hifadhi za jamii na hatimaye kukosa mafao yao.
Idadi kubwa ya wananchi wa Uganda wanakosa umoja na vyama vinavyoshughulikia mahitaji ya baada ya kustaafu kama vile huduma ya afya, makazi bora na mtiririko wa pesa unaotegemewa.
Hata wale waliotengwa na mifuko hii hutegemea mipango isiyo rasmi na rasilimali za familia ili kuishi. Tatizo ni kwamba, kama ilivyo katika maeneo mengine ya dunia ambapo uwiano wa utegemezi unapungua, shinikizo za kijamii zinafanya kuwa vigumu kwa makundi ya wastaafu barani Afrika kutegemea mipango ya familia na isiyo rasmi kwa ajili ya maisha endelevu.
Kimsingi, wataalamu wanapendekeza mapitio ya mifumo ya kisheria ili kuwaweka wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi chini ya usimamizi wao pamoja na usaidizi wa serikali kupitia mipango ya kifedha kama vile misamaha ya kodi na michango inayolingana ili kukusanya akiba ya kustaafu.
Muwanga Muhammad Kivumbi, mchumi kutoka Uganda na mwakilishi wa kaunti ya Butambala, anaamini kuwa mataifa ya Afrika ambayo tayari yana mifumo ya hifadhi ya jamii inayofanya kazi yanaweza kujadili namna ya kupanua wigo wa pensheni ili kujumuisha wale ambao hawajalipwa.
"Hata hivyo, kwa nchi kama Uganda na nyingine nyingi ambapo ufikiaji ni asilimia 10 tu, ni vyema majadiliano hayo kuendeshwa tofauti," anaiambia TRT Afrika.
"Huwezi kuzungumza juu ya kupanua wigo wa kitu ambacho hakipo. Tunahitaji kukiri kwamba mfumo wetu wa pensheni una ulakini, hivyo ni vyema tuangazie ukubwa wa mtanziko ambao tunakabiliwa nao na kuja na suluhu za kudumu."
Kubadilisha Fikra
Lydia Mirembe, meneja ushirika na umma wa URBRA, anasisitiza umuhimu wa kubadilisha fikra hasa kwenye maamuzi ya kufanya kabla ya kustaafu.
"Serikali iliwezesha mfumo wa kisheria na udhibiti kwa kuanzisha URBRA. Jukumu sasa ni la watu binafsi kutafakari maisha yao ya baadaye, kuchukua fursa ya mfumo huo na kujiandaa kwa kustaafu," anafafanua.
"Hii haimaanishi kuwa ninawaondolea wajibu waajiri. Mfumo wa kisheria uliopo unawalazimu kutuma michango ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria."
Asiimwe Aine, mwajiriwa kutoka sekta ya umma, ni miongoni mwa walimu wanaohofia mishahara yao midogo kuwa kikwazo cha kufurahia maisha baada ya kustaafu.
"Unapojiondoa kwenye mifuko ya hifadhi baada ya kudunduliza akiba yako ya muda mrefu, kuna uwezekano mdogo sana kwamba mkoba wa kustaafu utadumu kwa miaka kumi," anaiambia TRT Afrika.
Wakati teknolojia na uboreshaji wa mitindo ya maisha ikichangia kuongeza matarajio ya kuishi, bado Asiimwe anaona ni nusu tu ya vita iliyoshinda.
" Kwa kuanzia, serikali inapaswa kuimarisha na kuipa nguvu Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwani, kwa kiasi kikubwa itapunguza matumizi katika huduma za afya," anasema.