Ofisi ya Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta imeeleza wasiwasi kuwa juhudi za mchakato wa amani unaoongozwa na Kenyatta hazijazingatiwa katika mzozo unaoendelea nchini DRC.
" Mchakato wa amani wa Nairobi, licha ya kuwa ulisitishwa kwa muda, unasalia kuwa mchakato muhimu wa mazungumzo na utatuzi wa migogoro mashariki mwa DRC. Mratibu anaendelea kujitolea kutafuta njia za amani, kwa ushirikiano na serikali ya DRC, washirika wa kikanda, na wadau wa kimataifa," Kanze Dena msemaji wa ofisi ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta amesema.
Mchakato wa Nairobi ( Nairobi Process) kama unavyofahamika ni mchakato unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mpango wa amani wa kikanda unaolenga kutatua mzozo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ulizinduliwa mnamo Aprili 2022, kwa msingi wa kanuni za ujumuishaji, mazungumzo, umiliki, uongozi wa kikanda na usaidizi wa kimataifa huku Uhuru Kenyatta akiwa mjumbe maalum.
Chini ya mchakato huu viongozi wa EAC ambapo DRC ni mwanachama waliamua kupeleka Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) Mashariki mwa DRC mnamo Novemba 2022 kwa lengo la kurejesha amani na utulivu, dhidi ya kikundi chenye silaha cha M23.
Kwa sasa mchakato wa Umoja wa Afrika wa kuleta amani DRC unaoongozwa na Rais wa Angola Joao Lourenco ndiyo ambao unaonekana kupewa kipaumbele.
" Mratibu wa mchakato huu ana imani thabiti kwamba michakato miwili ya Luanda na Nairobi ina mipango mikubwa zaidi ya utatuzi na kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC. Michakato hii miwili ni ya kuridhisha na inawiana." ofisi ya Rais mstaafu Kenyatta imesema.
" Ni kupitia tu uratibu wa karibu wa mazungumzo ya pande mbili kati ya Rwanda na DRC na Mchakato wa Mazungumzo na Mikutano ya Ndani ya DRC ndipo mgogoro huu unaweza kupata suluhu yenye tija," ofisi imeongeza.