Ndugu hao wanatumia sanaa yao kuonesha mitindo tofauti na ya kushangaza./Picha: Ramadhani Brothers/AGT

Na Charles Mgbolu

Fadhili Ramadhani (26) na Ibrahim Jobu (36), wacheza sarakasi wanaounda kundi maarufu la 'Ramadhani Brothers' kutoka Tanzania, wamepania tena kutwaa taji la onesho la America’s Got Talent (AGT) baada ya kuingia kwenye orodha ya 10 bora ya makala Fantasy League.

Ndugu hao wamejizoelea umaarufu duniani kupitia mitindo yao tofauti na ya kushangaza wawapo jukwaani.

Wanasarakasi hao wamekuwa wakioanisha mitindo yao kwa mpangilio maalumu, kitu ambacho kimewaacha majaji wa shindano hilo midomo wazi.

‘’Muitikio ulikuwa ni wa kushangaza, ni kama mashabiki walihitaji kuona vitu vingi zaidi kutoka kwetu, tukajisemea. ' Huu ni mwanzo tu. Kwa sasa inabidi twende mbali zaidi',’’ alisema Fadhili katika mahojiano na watangazaji wa onesho la AGT, muda mfupi baada ya kuingia hatua hiyo.

'Ni ndoto kwetu'

‘’Hii ni kama ndoto kwetu,’’ aliongeza Ibrahim kabla Fadhili hajaendelea. ‘’Tunataka tulale huku tumevaa viatu!’’

Kwa mara ya kwanza, ndugu hao walishiriki kwenye msimu wa 18 wa AGT, uliofanyika kutoka mwezi Mei mpaka Septemba 2023, na kushika nafasi ya 5.

Ndugu hao walimaliza katika nafasi ya 5 katika shindano la AGT mwaka 2023. Picha: Ramadhani Brothers

Akiwa amehamasika na vipaji vya ndugu hao, mmoja wa majaji na mtangazaji Heidi Klum,aliamua kuwaweka kwenye ligi ya fantasy na hivyo kuwapa vigezo vya kuweza kushiriki kwenye mfululizo wa ligi ya Fantasy, iliyowakutanisha washindi wa zamani na mashabiki lukuki wa shindano hilo.

Ligi ya Fantasy ilianza kuoneshwa Januari 1, huku washiriki wote wakinuia kufikia hatua ya nusu fainali.

Wizi

Hata hivyo, jaji kutoka Canada Howie Mandel, aliamua 'kumuibia' Heidi ndugu hao wawili, na kuwapeleka katika hatua ya nusu fainali.

Katika hatua hiyo, ndugu hao walionesha mitindo tofauti ya kustaajabisha, ikiwemo na ile ya kupanda ngazi iliyosimamishwa jukwaani, huku wakiwa wamebebana vichwani.

Mitindo ya namna hii ndiyo iliyowapeleka ndugu hao katika hatua ya 10 bora.

‘’Tunatokea Tanzania na tulizaliwa na vipaji hivi ila hatukujua wapi pakuvionesha. Tunashukuru sana,’’ alisema Fadhili kwenye kipande cha picha mjongeo kilichowekwa na AGT kwenye mtandao wa YouTube.

Fainali ya ligi ya AGT Fantasy itafanyika Jumatatu, Februari 19 na mshindi atajinyakulia kitita cha dola za kimarekani 250,000.

TRT Afrika