Na Dayo Yussuf
Mitandao ya kijamii imejaa wito wa maandamano katika mataifa mbalimbali barani Afrika.
Ni jambo ambalo linawaacha wengi katika mshangao huku wakitazama vijana hao wakikabiliana na serikali zao.
Wimbi la maandamano yaliyoanza nchini Kenya na kuenea polepole katika mataifa mengine barani ni kipimo cha uchovu wa vijana.
Wanasema wamechoshwa na maovu yale yale ya kundi dogo la wanaotawala.
Nyimbo zile zile za ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma, upendeleo, ukosefu wa ajira na kadhalika.
‘’Nafikiri sasa kuliko wakati mwingine wowote, vijana wana ufahamu wa kisiasa na wanazingatia siasa,’’ asema Mike Muchiri, mwanaharakati kijana jijini Nairobi. ‘’Tumesoma na tunafahamu vyema kila kitu kinachoendelea katika ulingo wa siasa. Tunaelewa jinsi kila sekta, kila wizara inavyofanya kazi na jinsi michezo hii ya kisiasa inavyochezwa,’’ Muchiri anaiambia TRT Afrika.
Nchini Kenya vijana ambao wamekuwa wakiandamana kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, wanaapa kuendelea na msukumo huo hadi, kama wanavyosema, watakapoona mabadiliko ya kudumu.
Matatizo yanayofanana Afrika
Vijana wa Uganda pia wamefanya jaribio lao la kwanza katika maandamano hayo na nchini Nigeria serikali inafahamu kuhusu maandamano hayo yaliyopangwa na tayari inafanya baadhi ya makubaliano.
Siku chache kabla ya maandamano ya nchi nzima kuhusu utawala mbovu na gharama kubwa ya maisha, serikali ya Nigeria ilitoa ajira kwa vijana wake katika kampuni ya mafuta ya serikali na ruzuku ya mabilioni ya naira miongoni mwa motisha nyingine ili kukatisha tamaa hatua hiyo.
Ingawa wito wa kuchukua hatua bado unaendelea, angalau kwa sasa.
Kwa hiyo wanapoingia mitaani na ni pale wakifanikiwa kufika kwenye ofisi husika, labda bungeni au ofisi ya rais wanaenda kudai nini ?
‘’Jambo la kwanza ni utawala bora,’’ anasema Dk Bello Galadanchi, mwalimu na mshauri nchini Nigeria. ‘’Wanataka kweli serikali yenye uwazi ambayo ina mwelekeo wa watu,’’ anaiambia TRT Afrika.
Kwa kweli mambo yanaweza kutofautiana kutoka nchi hadi nchi, lakini utashangaa ni ngapi kati yao yanafanana.
Huduma ya afya, bima ya afya na uajiri wa madaktari na wauguzi zaidi huchukua nafasi ya juu katika orodha hiyo huku nchi nyingi zikililia hali mbaya katika hospitali za umma.
Hii ilichangiwa na utamaduni wa viongozi wengi wa serikali kukimbilia nchi za magharibi kwa matibabu kwa kutibu jamaa na familia zao.
Fursa za ajira kwa vijana wanaohitimu pia zinavuma katika bara zima.
Afrika ina idadi ndogo zaidi ya watu duniani, ikiwa na asilimia 70 ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara chini ya umri wa miaka 30.
Afrika bado iko nyuma katika ukosefu wa ajira huku nchi kama Afrika Kusini zikirekodi viwango vya juu zaidi kwa 33.5% huku nchi kama Nigeria na Kenya zikirekodi zaidi ya 5% kwa wastani.
Vijana walio wengi Afrika
Wachambuzi wanasema kupuuza demografia hii itakuwa katika hatari yao wenyewe.
Iwapo viongozi wa sasa ambao wengi wao ni kutoka vizazi komavu hawajumuishi vijana katika sera na utawala, kuna uwezekano mkubwa wa kuja na kulitwaa kwa nguvu.
Gharama kubwa ya maisha pia inasikika kuvuka mipaka.
‘’Maisha ni ghali sana hivi sasa, hasa chakula,’’ Dk Bello aliambia TRT Afrika. '’Kiwango cha mfumuko wa bei ni karibu 300%, na mishahara haiwezi kumudu milo mitatu kwa siku kwa watu wengi,’’ anasema.
Malalamiko mengine ya vijana hao ni kuondolewa kwa rushwa na kuondolewa madarakani kwa viongozi waliohusushwa na ufisadi, elimu ya bei nafuu na yenye ubora wa mifumo ya kidemokrasia ya serikali.
Kumekuwa na maafikiano na serikali ya Kenya baada ya kuanza kwa maandamano hayo. Rais wa Kenya William Ruto alitoa matangazo ya kurekebisha haraka ili kusaidia kutuliza hali ya wasiwasi.
Lakini wachambuzi wanasema hii haitoshi. Wengi wa vijana wanaangalia mabadiliko ya muda mrefu, endelevu zaidi.
‘’Vijana sasa wanafahamu sana kile wanachotaka sasa na kile wanachotaka kwa siku zijazo za karibuni na mbeleni,’’ Mike Muchiri anaiambia TRT Afrika.
Madai hayo si mapya. Viongozi wengi waliingia madarakani na kuahidi kutoa mambo yale yale katika ilani zao.
Lakini sasa, wanasema hakuna pesa za kufadhili mambo haya.
Lakini mtazamo wa chuki na kutokujali unaoonyeshwa na viongozi hao hao haujakaa vizuri na vijana.
Kulingana na vijana hao, ni suala la vipaumbele, wanaonekana kuweka maslahi yao kwanza mbele ya maslahi ya taifa.
‘’Unaweza kuona kwamba vijana wanadai mabadiliko ya kimfumo. Labda baadhi yao wanaweza wasijue ni nini hasa wanachotaka katika siku zijazo, lakini jambo moja kwa hakika ni kwamba hawataki mambo yaendelee kama yalivyo sasa. Wanadai mabadiliko,’’ Dk Bello anasema.