Marekani ilisasisha ushauri wake wa usafiri kwa Uganda ikitaja hatari za vurugu kutokana na uhalifu, ugaidi na sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Hata hivyo hili halikuwashangaza wengi. Marekani imekuwa ikitoa mashauri haya kiholela, ambayo wachambuzi wanasema yamepoteza maana yake.
‘’Mashauri haya ya usafiri yanayotolewa na nchi za magharibi hayana maana yoyote,’’ anasema Dk. Adams Bornah, mtaalam wa usalama nchini Ghana.
‘’Wanatoa kila robo mwaka au mara mbili kwa mwaka, lakini hawazuii chochote. Wanasababisha tu mkanganyiko na watu bado wanasafiri mara kwa mara kwenda katika nchi zilezile wanazoshauriwa kuzipinga.’’ Anaongeza.
Ushauri wa kusafiri hutolewa zaidi na nchi zilizoendelea ili kuwaonya raia wao juu ya wapi pa kwenda na wapi wasiende. Wanashauri jinsi ya kuishi katika maeneo fulani au karibu na watu fulani kulingana na uchambuzi wao wa hali ya usalama katika maeneo hayo.
Hata hivyo baadhi ya nchi za magharibi, Marekani haswa imekuwa ikitoa ushauri huu bila mpangilio, wakati mwingine kuzua maswali juu ya nia yake halisi.
Dk Adams anasema mara nyingi unakuta hali ni mbaya zaidi kwao wenyewe kuliko pale wanaponyooshea vidole.
‘’Kwa mfano wanawaambia watu wasiende sehemu za Afrika, lakini umeona New York au Washington DC, vurugu za huko ni mbaya zaidi kuliko zinazotokea Burkina Faso. Wana changamoto zao wanapaswa kuzingatia.’’ Anaongeza. ‘’Kuna visa vingi vya unyanyasaji wa visu mjini London kuliko Somalia.’’
Marekani imetoa zaidi ya mashauri 40 ya usafiri katika sehemu mbalimbali za dunia mwaka huu pekee. Hata hivyo, kulingana na mchambuzi wa masuala ya usalama Dkt Adams, watu hao hao wanaodai kuwalinda hawaamini neno lao.
‘’Nenda tu Kaskazini mwa Nigeria, au hata sehemu za Cameroon na Somalia. Tazama kuna Wamarekani wangapi. Huwezi kuwazuia watu kuzunguka.’’ Anasema Dk Adams.
Wachambuzi pia wanasema baadhi ya mashauri haya ya usafiri ni njia ya kuzishawishi nchi zinazoendelea kufuata sera zake.
‘’Nionavyo mimi, watu hawa wanaleta mkanganyiko tu huku wakijificha nyuma ya ulinzi na usalama wa kimataifa,’’ anasema Dkt. Adams. ‘’Unapotofautiana nao au wanahisi hauendi sambamba na mstari wanaotaka wao, wanakuja na matamshi haya ili kuwasaidia kusukuma ajenda zao.’’
Marekebisho mapya ya ushauri wa usafiri wa Marekani yanarejelea sheria ya hivi majuzi ya kupinga mapezi ya jinsia moja iliyopitishwa na bunge la Uganda ambayo inatoa adhabu kali.
Ofisi ya idara ya serikali ya Marekani ya huduma za kibalozi ilichapishwa kwenye tovuti yake: ''Sheria ya Mei 2023 ya Kupinga mapenzi ya jinsia moja inaongeza hatari kwamba watu wa LGBTQI+, na wale wanaochukuliwa kuwa LGBTQI+, wanaweza kufunguliwa mashtaka na kuhukumiwa kifungo cha maisha au kifo kulingana na masharti katika sheria, na wanaweza kushurutisha kuripoti kwa lazima kwa polisi iwapo watashukiwa kufanya au kukusudia kufanya vitendo vinavyokiuka sheria, na wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji au kushambuliwa na maafisa wa usalama.''
Hata hivyo Rais Museveni amerudia kutetea sheria hiyo ambayo alitia saini akisema ‘’Nchini Uganda, mapenzi ni siri, hata mapenzi ya jinsia tofauti. Kwa hiyo ikiwa mpenzi wa jinsia moja atajiweka mwenyewe au kutafuta usaidizi kwa siri kutoka kwa madaktari au makasisi, haitavunja sheria hii.’’
Tangu Mei wakati Rais Museveni alipotia saini mswada wa Kupinga Ushoga kuwa sheria, nchi hiyo imepokea ukosoaji kutoka kwa nchi mbalimbali za magharibi ikiwa ni pamoja na vitisho vya kuwekewa vikwazo na kunyimwa ufadhili muhimu.
Rais wa Marekani Joe Biden pamoja na mkuu wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia wamekashifu sheria hiyo, na kuonya kuwa misaada ya kigeni na uwekezaji kwa Uganda inaweza kuhatarishwa iwapo sheria hiyo haitafutwa.
Kulingana na mtaalamu wa masuala ya Usalama Dkt Adams, viongozi wa Afrika wanapaswa kuwa na msimamo thabiti ili kuepuka vitisho kutoka kwa nchi tajiri.
‘’Viongozi barani Afrika wanatakiwa kuwa na ujasiri wa kutosha kupinga kusukumwa. Wanahitaji kuwaambia watu wao ukweli kuhusu hali ya nchi hizi za magharibi pia. Hawako salama jinsi wanavyodai kuwa.’’ Anasema Dk, Adams.