Nini kifanyike kudhibiti maambukizi ya Ebola Afrika ?

Nini kifanyike kudhibiti maambukizi ya Ebola Afrika ?

Mwaka wa 2023 ulianza bila nchi yeyote barani kutangazwa kuwa na visa vya Ebola
Uganda ilitangazwa kuwa haina tena maambukizi ya virusi vya Ebola mapema mwaka huu  / Photo: AP

Na Coletta Wanjohi

Kitengo cha Kudhibiti Magonjwa cha Umoja wa Afrika, Africa CDC, kinasema ni lazima eneo la Afrika Mashariki kuwa chonjo ili kuepuka kuwepo kwa visa vya Ebola katika eneo hilo mwaka huu wa 2023.

Dalili kuu za Ebola ni pamoja na homa kali inayoambatana na kuvuja kwa damu.

Mapema mwaka huu Uganda ilitangazwa kuwa haina tena wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya Ebola.

Wakati huo huo, nchi kama Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Rwanda, na Sudan Kusini ziliwekwa katika hali ya tahadhari wakati Uganda ilipotangaza kuzuka kwa ugonjwa huo mnamo tarehe 20 Septemba, 2022.

Takribani dola milioni 3 za kimarekani zilitengwa na Shrikia la Afya Duniani, (WHO) ili kuwajengea uwezo na kuwasaidia kukabiliana na janga hilo.

Nchi ya DRC pia ilitangazwa kutokuwa na virusi vya Ebola mnamo tarehe 27, mwezi Septemba, 2022 baada ya kukabiliana na mlipuko wake kwa mara ya 15.

Kaimu Mkurugenzi wa Afrika CDC, Dkt. Ahmed Ogwell anasema udhibiti madhubuti wa milipuko unategemea urahisi wa kuifikia jamii.

"Unapoweza kufikia jamii, unaweza kuwashirikisha moja kwa moja, mara kwa mara, na kufuatilia ni nini ushirikiano huo unakupa," Ogwell aliiambia TRT Afrika katika mkutano na waandishi wa habari na kuongeza, "Nchini DRC, imekuwa ni changamoto kidogo hasa katika maeneo ambayo yamekuwa na vita, na ndiyo sababu kulikuwa na ukaidi kidogo wa ugonjwa huu katika sehemu hiyo ya Afrika."

Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa jitihada katika ngazi ya kimataifa.

"Kila kunapokuwa na shida kuna msaada mwingi ambao huja. Ikiwa haijaratibiwa haikupi matokeo ya haraka. Nchini Uganda uratibu ulikuwepo kuanzia siku ya kwanza ya ugonjwa huu kugunduliwa, waziri wa afya ndiye alikuwa akisimamia mchakato huo, na aliuratibu hadi mwisho wa mlipuko huo.”

Changamoto ya upatikanaji wa chanjo dhidi ya Ebola

Mwaka 2019 Utawala wa Chakula na Dawa wa Marekani uliidhinisha chanjo ya Ervebo ambayo inasema imegundulika kuwa salama na kinga dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Zaire ambayo hukumba DRC.

Lakini bado hakuna chanjo dhidi ya virusi aina ya Sudan ambavyo huikumba Uganda mara kwa mara. Asili ya virusi hivi bado haijajulikana.

Kwa upande wake, WHO, katika uchambuzi wa mlipuko huo inasema huu ni mlipuko wa kwanza wa virusi vya aina ya Sudan nchini Uganda tangu mwaka 2012. Kwa jumla ni mara ya tano ya virusi hivi kushambulia Uganda.

Virusi hivyo vimeripotiwa nchini Sudan mara tatu.

Umuhimu wa jamii kutoa taarifa

Dkt. Ogwell, anaiambia TRT Afrika kwamba ili kuzuia milipuko yoyote ya siku zijazo ni lazima raia wawe tayari kutoa ripoti pindi wanapokuwa na shaka yoyote.

"Milipuko huanza na kuishia katika jamii. Ikiwa jamii ipo katikati ya kutambua mlipuko, basi tunafahamu kuhusu ugonjwa huo haraka. Iwapo jamii haiwezi kubaini kuwa kuna mlipuko au wanaposhuku magonjwa yoyote, na wanaficha kutoa maelezo, basi ugonjwa utaenea kwa watu wengi zaidi.” Ogwell anashauri.

Uganda inajiandaa kufanya majaribio ya kimatibabu kutathmini chanjo dhidi ya virusi vya ebola aina ya Sudan. Dozi za kwanza za chanjo moja kati ya tatu zilizofanyiwa majaribio ziliwasili nchini humo mnamo Desemba 2022.

Lakini bado majaribio hayajaanza kwasababu ni lazima kuwepo na idadi ya wagonjwa kiasi fulani kwanza, kulingana na shirika la afya duniani.