Mohamed Bazoum, yuko katika "hali nzuri" licha ya kuwa kizuizini bila umeme na kukosa mawasiliano na jamaa, mshauri wake wa zamani alisema Jumamosi.
Amadou N'Gade, alisema kuwa njia za mawasiliano za rais, haswa simu zake za rununu, hazifanyi kazi baada ya umeme kukatwa karibu wiki mbili zilizopita.
"Rais Mohamed Bazoum yuko katika hali ya furaha lakini hana mawasiliano tena na jamaa zake," Hamidou Amadou N'Gade, mshauri wa zamani wa rais aliyeondolewa alichapisha kwenye Facebook, huku akimnukuu daktari wa Bazoum aliyemzuru.
"Ni dharura, kwamba watekaji nyara waunganishe tena umeme katika nyakati hizi za joto na mbu. Chochote kinaweza kumtokea bila kuonekana au kusikika na macho au masikio ya ulimwengu wote na familia yake, "aliandika.
Ziara hiyo iliidhinishwa kufuatia kuongezeka kwa matakwa ya kimataifa ya kuachiliwa kwake.
Jamaa wa karibu wa Bazoum waliviambia vyombo vya habari kuwa daktari wake wa kibinafsi "alimletea chakula na dawa" Jumamosi na aliweza kuzungumza naye, pamoja na mke wake na mwanawe.
Ziara hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Bazoum tangu ile ya Rais wa mpito wa Chad Mahamat Idriss Deby, tarehe 31 Julai.
Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Victoria Nuland alizuiwa kuonana na Bazoum alipotembelea Niamey Agosti 7, baada ya kufanya mazungumzo "ya wazi na magumu" na maafisa wa chini.
Ripoti za hivi majuzi zilikuwa zimetoa picha mbaya ya afya ya Bazoum tangu kupinduliwa kwake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alishutumu "hali mbaya ya maisha" ambayo Bazoum na familia yake wanasemekana kuishi.
Siku ya Ijumaa, Shirika la kimataifa la kutetea haki la Human Rights Watch,liliwataka viongozi wa mapinduzi wawahakikishie usalama na ustawi wa Bazoum, familia yake na wengine ambao wanazuiliwa.
Viongozi wa mapinduzi ya Niger, wanamtesa Bazoum, familia yake na watu wengine wasiojulikana kinyume na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu
Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), katika mkutano wa dharura Alhamisi, katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja, walitishia kutumia nguvu kurejesha utulivu wa kikatiba na kurejesha Bazoum.
Jenerali Abdourahamane Tchiani, kamanda wa zamani wa walinzi wa rais wa Niger alijitangaza kuwa mkuu wa serikali ya mpito baada ya jeshi kumuondoa Bazoum.