Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno alienda Niger kwa mkutano na viongozi wa waliofanya mapinduzi ya kumuondoa rais Mohamed Bazoum/ Picha: Mahamat Deby/Twitter

Wakuu wa kijeshi wa Afrika Magharibi wamekubaliana kufanya mpango wa kuingilia Niger wakati muda wa mwisho unakaribia kwa serikali ya nchi hiyo kumrejesha madarakani kiongozi aliyechaguliwa Mohamed Bazoum.

Viongozi wa ECOWAS Jumapili iliyopita waliweka vikwazo vya kibiashara na kifedha na kuwapa viongozi wa mapinduzi wiki moja kumrejesha madarakani rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia la sivyo wakabiliane na uwezekano wa matumizi ya nguvu.

"Mipango ya mahitaji yote ambayo yatatumika katika uingiliaji kati wowote hatimaye yamekamilika, ikiwa ni pamoja na rasilimali zinazohitajika, na ikiwa ni pamoja na jinsi na lini tutapeleka kikosi," kamishna wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah alisema Ijumaa.

"Tunataka diplomasia ifanye kazi, na tunataka ujumbe huu ufikishwe kwa wanajeshi waliofanya mapinduzi Niger, wazi kwamba tunawapa kila fursa ya kubadili walichofanya," aliongeza.

Wakuu hao wa kijeshi walikuwa wakikutana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja kujadili njia za kukabiliana na mzozo huo.

ECOWAS mapema wiki hii ilisema kwamba uingiliaji kati wa kijeshi katika Niger inayotawaliwa na junta ilikuwa "suluhisho la mwisho."

Uamuzi wa Chad

ECOWAS imeapa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya mapinduzi ambayo yameenea katika eneo lote tangu 2020, mengi yao chini ya shinikizo la uasi.

Mali na Burkina Faso zimeonya kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi katika jirani yao itakuwa sawa na "tangazo la vita" dhidi yao.

Wakati huo huo, Chad inasema haitaingilia kijeshi nchini Niger.

Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo alisema hayo kwenye televisheni ya taifa siku ya Ijumaa, huku Jumuiya ya ECOWAS ikiwa imepanga kumrejesha madarakani Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum.

Ingawa Chad si mwanachama wa ECOWAS, ina uhsirika mkuu na ECOWAS , ikiwa kiongozi wa mpito wa Chad Mahamat Deby alihudhuria mkutano wa ECOWAS kuhusu Niger wiki iliyopita . Deby pia alisafiri hadi Niger kutoa ujumbe wa ECOWAS kuhusu haja ya kurejesha utaratibu wa kikatiba.

Chad na Niger zinapakana na zote zimeathiriwa na uasi wa makundi yenye silaha yanayoharibu eneo la Sahel barani Afrika.

Kwa miongo kadha ailiyopita ECOWAS imetuma kikosi cha kikanda kusaidia kurejesha utulivu katika mataifa ya Afrika Magharibi yaliyokumbwa na msukosuko wa kisiasa. Mnamo mwaka wa 2017, ilituma wanajeshi 7,000 nchini Gambia kutoka nchi jirani ya Senegal kumlazimisha rais Yahya Jammeh kwenda uhamishoni na kuacha urais kwa Adama Barrow, ambaye alimshinda katika uchaguzi.

TRT Afrika