Niger yawavua uraia watu tisa  walioshirikiana na Rais wa zamani Bazoum

Niger yawavua uraia watu tisa  walioshirikiana na Rais wa zamani Bazoum

Watu hao wanashutumiwa kwa kufanya makosa makubwa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na mataifa ya kigeni.
Jeshi la Niger lilichukua mamlaka mnamo Julai 2023, na kumuondoa Rais Mohamed Bazoum ambaye bado yupo kizuizini/ Picha Wengine 

Serikali ya Kijeshi ya Niger imewafutia uraia watu tisa ambao walikuwa washirika wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum wa Niger.

Walioathirika ni pamoja na Waziri wa zamani katika Ofisi ya Rais, Rhissa Ag Boula, ambaye kwa sasa yuko uhamishoni nchini Ufaransa. Watu wengine wanane walioathirika pia wanaishi nje ya nchi, kulingana na vyombo vya habari vya mtandaoni ActuNiger.

Wamepokonywa kwa muda uraia wao wa Niger kwa "makosa makubwa yanayohatarisha usalama wa taifa,” ilisema amri iliyotiwa saini siku ya Alhamisi na kiongozi wa nchi hiyo, Jenerali Abdourahamane Tiani.

Amri hiyo "inalenga kuwaadhibu watu wanaohusika katika vitendo vya ugaidi, uhaini, na ujasusi wakishirikiana na mataifa ya kigeni," kulingana na taarifa ya serikali.

'Vitendo vya uadui'

Mamlaka ya uongozi wa kijeshi nchini humo inasema, inaongeza juhudi "kulinda maslahi ya kimkakati ya nchi na kudumisha utulivu wa umma."

Watu wanaolengwa na vikwazo hivyo wanatuhumiwa kufanya au kuhimiza vitendo vinavyoweza "kuhatarisha maslahi ya kimkakati ya Niger".

"Makosa haya ni pamoja na ushirikiano na mataifa ya kigeni, kijasusi kwa vitendo vya uadui dhidi ya serikali, uhaini, na kukandamiza jeshi la taifa."

Jeshi la Niger lilichukua mamlaka mnamo Julai 2023, na kumuondoa Rais Mohamed Bazoum, ambaye amekuwa kizuizini tangu wakati huo.

TRT Afrika