Umoja wa Afrika Magharibi wa ECOWAS unalenga kutuma kamati ya bunge nchini Niger kukutana na viongozi wa mapinduzi, ambao walichukua mamlaka mwezi uliopita na kisha kupinga shinikizo za kurejesha utawala wa kiraia, msemaji wa bunge alisema.
Mpango huo unakuja siku ya Jumamosi baada ya jeshi la Niger kumzuilia Rais Mohamed Bazoum mwezi uliopita, na kuvunja serikali iliyochaguliwa, hatua iliyopelekea kulaaniwa na mataifa yenye nguvu ya kikanda.
ECOWAS imesema imeunda kikosi cha kijeshi ambacho inatishia kukituma kama suluhu la mwisho iwapo mazungumzo yatashindikana.
Hata hivyo, viongozi wa mapinduzi yaliyoongozwa na Jenerali Abdourahamane Tchiani, wamepinga shinikizo za kidiplomasia kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Marekani na mataifa mengine, na hivyo kuibua hali ya mzozo zaidi katika eneo maskini la Sahel la Afrika Magharibi, ambalo tayari linagubikwa na uasi mbaya wa wanamgambo.
Hatarini sio tu hatima ya Niger, ambayo ni mzalishaji mkuu wa madini aina ya Uranium na mshirika wa Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo, lakini pia ushawishi wa mataifa makubwa yenye maslahi ya kimkakati katika Afrika Magharibi na Kati, ambako kumekuwa na mapinduzi saba ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Wanajeshi wa Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Italia wako nchini Niger, katika eneo ambalo washirika wa ndani wa Al Qaeda na Daesh wameua maelfu na mamilioni ya watu kuyahama makaazi yao.
Wakati huo huo, ushawishi wa Urusi umeongezeka sana nchini Niger na kutanuka eneo zima.
Bunge la ECOWAS lilikutana Jumamosi kujadili hatua zaidi nchini Niger.
Hakuna uamuzi uliotolewa, lakini inaaminiwa kuwa, bunge liliunda kamati ambayo inapanga kukutana na Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ambaye anashikilia uenyekiti unaozunguka wa ECOWAS, ili kupata kibali chake cha kwenda Niger.
Mataifa ya Magharibi yenye nguvu yanahofia ushawishi wa Urusi unaweza kuongezeka ikiwa Junta la nchini Niger litafuata nyayo za nchi jirani za Mali na Burkina Faso, ambazo ziliwaondoa wanajeshi wa wakoloni wake, Ufaransa baada ya mapinduzi katika nchi hizo.
Mali, tangu wakati huo, imeungana na mamluki kutoka Urusi, Wagner, hatua ambayo imeambatana na kuongezeka kwa ghasia huko.
Pia, imekiondoa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, ambacho wachambuzi wa masuala ya usalama wanahofia kinaweza kusababisha mzozo zaidi.