Na Emmanuel Onyango
Watu wengi nchini Kenya na kwingineko bado wako katika mshtuko na kutoamini huku miili zaidi ikitolewa kufuatia vifo vya umati vinavyohusishwa na shughuli za kundi la waasi katika kaunti ya Kilifi kusini-mashariki mwa nchi.
Hali ya kutisha iliyojitokeza kwa mara ya kwanza mwezi wa Aprili, inatia uchungu zaidi jamaa za wahasiriwa wakiwemo wanawake na watoto - ambao inadaiwa waliambiwa na kiongozi huyo wa madhehebu wajinyime njaa ili wamwone 'Yesu.'
"Hatujawahi kuona dini ambapo wanawake wanaonyonyesha watoto wachanga wanalazimishwa kufunga kula," Zipporah Kwamboka, ambaye aliwaona ndugu zake mara ya mwisho mwaka 2021, anaiambia TRT Afrika.
Awamu ya tatu ya uchimbaji na ufukuaji wa miili inayohusishwa na ibada ya njaa lilianza wiki hii karibu na msitu wa Shakahola.
Idadi ya vifo imepanda hadi zaidi ya 254 na mamlaka inahofia mamia zaidi bado wametawanyika katika msitu mkubwa karibu na mji wa pwani wa Malindi.
Vifo hivyo vinaonekana kusababishwa na njaa, lakini baadhi ya waathiriwa - ikiwa ni pamoja na watoto - walikuwa na dalili za kunyongwa au kukosa hewa, kulingana na madaktari wa magonjwa walioteuliwa na serikali.
Kusubiri kwa wasiwasi
Polisi wanaamini kuwa miili hiyo ni ya wafuasi wa Paul Nthenge Mackenzie, dereva wa teksi aliyegeuka kuwa kiongozi wa kiinjilisti wa Kanisa la Good News International, ambaye mafundisho yake yanasemekana kuhimiza tabia za kujinyima raha kama njia ya kwenda mbinguni.
Kwamboka akiwa na machozi anasema ndugu zake walikuwa wameuza mali ya familia yao kabla ya kujiunga na dhehebu hilo.
''Waliuza ardhi ya familia yetu na kusema wangenunua ardhi katika nchi jirani Tanzania. Lakini mwezi wa Aprili,mwaka huu tulipata habari kwamba walikuwa washiriki wa Kanisa la Good News International Church,” Kwamboka anasema.
Kwamboka ni miongoni mwa ndugu wa wahasiriwa wanaopiga kambi nje ya ofisi ya serikali mkoani humo na kusubiri taarifa za waliko wapendwa wao waliopotea.
Harakati za kiroho zenye mafundisho ya itikadi kali hapo awali, zimesababisha vifo vya watu wengi na mateso mengine ya washiriki wao katika sehemu za Afrika.
Lakini kisa cha hivi punde zaidi nchini Kenya kinaaminika kuwa mojawapo ya misiba mibaya zaidi inayohusiana na ibada potovu katika historia ya hivi majuzi katika bara hili, na kuongezeka kwa idadi ya vifo na siri inayoizunguka.
Sasa timu ya rais imeanza kubaini jinsi mapungufu katika sheria, kanuni na mwelekeo wa kijamii yaliruhusu Mackenzie kueneza mafundisho yake ambayo yanadaiwa kusababisha vifo vya watu wengi.
Mhubiri huyo hapo awali alikiri kuhubiri juu ya mwisho wa dunia. Ingawa amefika mahakamani, mashtaka halisi dhidi yake bado hayajawekwa wazi.
Maafisa walikuwa wamesema Mackenzie atashtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi kwa kutumia vibaya hisia za kidini kuwahadaa maelfu ya watu.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kwamba anakanusha makosa yanayohusiana na vifo vingi vya wafuasi wake.
Kivutio cha miujiza
Kiongozi wa ibada ya njaa, Mackenzie amekuwa kizuizini na mamlaka inasema uchunguzi unaendelea.
Mchungaji huyo alitumia kampuni yake ya runinga, ambayo pia huonyesha kwenye mtandao, kupata wafuasi kutoka maeneo ya ndani ya Kenya na nje ya mipaka ya nchi hiyo lakini viongozi wanasema baadhi ya mafundisho yake yalikuwa na msimamo mkali.
Alikuwa na uwezo wa kujua yote juu ya wafuasi wake ambao walihimizwa kwamba kazi yao duniani imefanywa na wanapaswa kufa ili kupata wokovu, kulingana na wale waliojitenga na kanisa.
Kiwango potovu cha hali ya kutisha kimewaacha Wakenya wengi wakishangaa kuhusu aina ya watu wanaojiunga na shughuli za ibada hiyo na jinsi kanuni za sasa zilivyoruhusu matukio ya msitu wa Shakahola kuendelea bila kutambuliwa kwa muda mrefu.
"Wengi wa watu ambao wanajipata katika vikundi kama hivyo wanapitia changamoto moja au nyingine," alisema James Mbugua, mtaalamu wa saikolojia wa ushauri nasaha katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene, nchini Kenya.
"Na haswa katika hali yetu ya Kenya ni udhaifu ambao wengi wetu hubeba ... na wanaposikia miujiza ambayo hufanyika mara moja bila shaka watavutiwa na vikundi hivi. Mafundisho yao yanahusu mahali pazuri zaidi kuliko anakotoka mtu ,” Mbugua asema.
Miongoni mwa maswala ambayo jopo kazi la rais italazimika kukabiliana nalo ni suala la uhuru wa kidini, ambao umewekwa katika sheria za Kenya, lakini ambao wengi sasa wanadai kuwa unatumiwa vibaya
Kenya ni nchi ya waumini waaminifu - asilimia 85 ni Wakristo huku asilimia 11 ni Waislamu kulingana na makadirio rasmi.
Mianya iliyotumika
Rais wa Kenya William Ruto amelaani mazingira yaliyosababisha vifo vya watu wengi na kuapa kuwa serikali yake itachukua hatua huku akikiri kudorora kwa kitaasisi katika kufuatilia shughuli za mashirika kama hayo ya kidini.
Sasa kuna ongezeko la wito wa kutunga sheria kwa ajili ya udhibiti bora wa shughuli za mashirika ya kidini na viongozi wao.
Baadhi wanataja kuwa mafanikio yaliyorekodiwa nchini Rwanda yenye sheria ambayo inahitaji viongozi wa kidini kuwa na kiwango fulani cha kitaaluma na kufaulu mtihani wa uaminifu .
Sheria hiyo pia inasema kuwa ruzuku na usaidizi mwingine wa kifedha kwa mashirika ya kidini lazima upitishwe kupitia benki. Hii ni kuhakikisha uchunguzi sahihi.
Lakini kudhibiti shughuli zinazohusiana na imani pia kuna uwezekano wa kukumbwa na misukosuko kutokana na hali ya kidini ya jamii.
Wachambuzi wanasema itakuwa mtihani mkubwa kwa jopokazi la serikali katika azma yake ya kuafikiana kuhusu mpango wa mageuzi ambao utalinda watu dhidi ya mafundisho na desturi zenye madhara za kidini.
Kwa wafuasi wa udhibiti, hakuna chaguo bora zaidi.
“Tunapozungumzia kanuni hatuzungumzii kubana ibada. Viongozi wa kidini wanafaa kufanya kazi ndani ya mipaka iliyoainishwa,” asema Dkt Mbugua. "Hili tukio la Shakahola, lilikuwa la muda mrefu na pengine tutakuwa na hali mbaya zaidi katika siku zijazo na uanzishaji wa sasa wa mashirika ya kidini. Tunahitaji kuwa waaminifu sisi wenyewe,” anaongeza.
Kwa Zipporah Kwamboka na jamaa wengine walioathiriwa kw anji moja au nyingine na ibada ya njaa, kipaumbele chao cha haraka ni kupata haki .
Wengi wao wanatafuta jibu kwa nini waliwapoteza wapendwa wao katika hali hiyo ya kusikitisha.