Ndege ya shirika la Air Tanzania, ambayo ilizuiliwa nchini Uholanzi mnamo Desemba 2022, imeachiliwa.
Ndege hiyo, Airbus A220-300 5H-TCH, ilikuwa imesimamishwa baada ya kampuni ya kibinafsi ya Uswidi, EcoEnergy Limited, kushinda kesi ya dola milioni 165 dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa alisema ndege hiyo ilitua nchini kutoka Uholanzi Julai 6, 2023.
Siku ya Jumamosi, Msigwa, ambaye alizungumza katika hafla iliyofanyika kaskazini mwa jiji la Arusha, alisema Tanzania na kampuni ya Uswidi zilifanya "majadiliano yenye mafanikio" ambayo yalifikia kilele cha kuachiliwa kwa ndege hiyo.
Alisema ndege hiyo inafanyiwa ukarabati ili iweze kutumika kibiashara na Air Tanzania.
Mgogoro wa ardhi
Kampuni ya EcoEnergy Limited, mwaka 2017, iliishtaki serikali ya Tanzania baada ya kufuta hati miliki ya ardhi iliyochukuliwa na kampuni hiyo ya kigeni.
Kampuni ya Uswidi, inayojishughulisha na huduma za viwanda vya kilimo, ilikuwa na mpango wa kuendeleza mradi wa mabilioni ya dola katika eneo la Bagamoyo, mashariki mwa Tanzania kabla ya hati miliki hiyo kufutwa mwaka 2016.
Serikali ya Tanzania ilisema sehemu hiyo ya ardhi ni mali ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, na kwamba hati miliki ilitolewa kwa njia isiyo ya kawaida.
Kampuni ya Uswidi, ambayo ilifanya kazi katika kiwanda cha kuzalisha umeme kwa miaka kumi, na kupata gharama ya thamani ya dola milioni 52, ilisikitishwa na uamuzi huo na kuwasilisha uvunjaji wa kesi ya mkataba, ikitaka fidia ya jumla ya dola milioni 165.
Mnamo Desemba 2, 2022, kampuni hiyo ilipata amri kutoka kwa mahakama ya Uholanzi ya kukamata ndege ya Air Tanzania baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa nchi hiyo.
Tanzania ilieleza nia yake ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Makubaliano ya hivi punde yaliyofikiwa kati ya Tanzania na upande uliolalamika - ambayo yalisababisha kuachiliwa kwa ndege - bado haijulikani wazi.