Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Wakati wakuu wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), watakapokutana siku ya Novemba 30 kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 25 ya jumuiya hiyo, jambo ambalo litakuwa linatawala vichwani mwao ni namna vikwazo vya biashara vinavyozidi kurudisha nyuma maendeleo ya jumuiya hiyo.
Hili si jambo geni, kwani imekuwa ni kitu cha kawaida kuona nchi wanachama ‘zikilinda vyao’, kwa maslahi yao, bila kujali maslahi mapana ya jumuiya nzima yenye jumla ya watu milioni 343.3.
Licha ya uwepo wa utashi wa kisiasa katika kuondoka vikwazo hivyo, bado tatizo linaendelea kuwa kubwa kwani baadhi ya nchi wanachama zinaendelea kukumbatia maslahi yao.
“Ni dhahiri kuwa vikwazo hivi vinachochewa na ukweli kwamba zipo nchi zinazoendelea kulinda maslahi yao, kulinda bidhaa zao zisizo na ushindani dhidi ya zenye ushindani kutoka nchi wanachama wengine,” anasema Kaimu Afisa Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Adrian Njau.
Ni kwa sababu hiyo, Njau anasisitiza haja ya sekta binafsi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa nchi wanachama wanaondokana na urasimu wa namna hiyo ambao unaongeza gharama za biashara na kutoa wigo kwa vikwazo ya biashara.
Kulingana ripoti ya mwaka 2023, jumla ya vikwazo 274 vimeshughulikiwa hadi kufikia sasa, huku kukiwa kumesalia na vikwazo 10.
Hata hivyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki bado inakabiliana na athari za vikwazo hivyo vinavyotokana na urasimu kwenye masuala ya forodha.
Kulingana na EABC, sababu za namna hiyo hudumaza na kudhoofisha biashara ndani ya ukanda wa EAC.
“Hali ni mbaya zaidi mipakani, kuna misururu mirefu ambayo kwa hakika inazidi kuathiri ufanyaji biashara wa pamoja kati ya nchi wanachama licha ya uwepo wa mifumo ya kukabiliana na vikwazo hivyo,”Njau anasema.
Kulingana na Kaimun Mtendaji huyo wa EABC, kuondoka vikwazo hivyo ni jambo moja, na kujitokeza kwa vikwazo kama hivyo tena, ni jambo lingine.
Hii ndio sababu jukwaa hilo linataka kuwepo na mifumo thabiti ambayo itaangazia tatizo hilo na kulikomesha mara moja.
Jumuiya ya Afrika Mashariki imeondoa vikwazo kwa raia wa nchi wanachama kuvuka mipaka ya taifa moja hadi jingine. Pamoja na hali hiyo, bado mambo si mazuri kibiashara.
Suala lingine ambalo linaonekana kuwa ni kizungumkuti kwa Jumuiya ya EAC, ni uanzishwaji wa sarafu moja, mpango ambao umesogezwa tena mbele hadi mwaka 2033.
Nchi wanachama wa EAC zilitia saini itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAMU) Novemba 2013.
Mkakati huo, ulikuwa uanze mwaka 2024 lakini ukahairishwa tena mpaka 2033.
EAMU iliweka msingi wa kuanzishwa kwa umoja wa fedha ndani ya miaka 10 na kuruhusu wanachama wa EAC kuunganisha sarafu zao taratibu hadi kuwa na sarafu moja ndani ya Jumuiya.
Mwezi Agosti mwaka huu, Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva alinukuliwa akisema kuwa licha ya vipengele vya mpango huo kuanzishwa, bado nchi wanachama wameendelea kutofautiana kuhusu vipengele vingine.
Vipengele hivyo ni pamoja na utengenezaji wa nyaraka za kisheria kwa ajili ya kuanzisha taasisi zitakazosaidia Umoja wa Fedha.
Kwa mujibu wa Nduva, nyaraka hizo zipo katika hatua mbalimbali za mchakato wa kupitishwa.
Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, bado EABC ina matumaini kuwa siku moja EAC itakuwa na sarafu yake.
“Lengo hili linawezekana kabisa kutimia iwapo nchi wanachama zitaonesha utashi wa kweli wa kisiasa,” anaiambia TRT Afrika.
Kuhusu kuoanisha sera za kifedha, Njau anasema kuwa benki kuu katika nchi wanachama zimepiga hatua kubwa kuhakikisha kuwa suala hilo linapata msukumo.
“Bado tuna imani kuwa kuongeza kwa muda huo kutatupa nafasi ya kujenga taasisi imara na madhubuti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa sarafu moja.”