Muonekano wa chumba ndani ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, huko The Hague Uholanzi. Picha: ICJ 

Na Sylvia Chebet

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Magwiji wa sheria na wataalamu wengine kutoka mashirika makubwa ya kimataifa wameanza kupimana mbavu katika shauri la Afrika Kusini dhidi ya Israeli ambalo limeanza kusikilizwa kwenye Mahakama hiyo, iliyoko The Hague, Uholanzi.

Katika jalada lenye kurasa 84 la shauri hilo, Afrika Kusini inaishutumu Israeli kwa mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Msingi wa kesi yake upo katika maelezo kamili ya vitendo vya mauaji ya Israel kufuatia shambulio dhidi ya kundi la Hamas, lillitokea Oktoba 7, mwaka jana.

Kesi hiyo inaangazia mauaji na uharibifu mkubwa uliofanywa na Israeli, ikiwa ni pamoja na kuikatia mji wa Gaza, huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, chakula, dawa na mafuta.

Katika kesi hiyo, Afrika ya Kusini imeazimia kukomesha mashambulizi ya kijeshi ya Israeli ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 23,000, wakiwemo watoto 10,000.

Pande zote mbili ziliwasilisha hoja zao mbele ya majaji mjini The Hague jana, na zitaendelea tena leo. Jopo la majaji 17, linategemewa kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya shauri hilo kwenye mahakama hiyo.

"Madhali hili ni suala la kisiasa, kila hoja itakuwa na uzito wake kwenye maamuzi haya," mtaalamu wa sheria Nabil Orina anaiambia TRT Afrika, akiongeza kuwa "majaji tisa zaidi watahitajika kukamilisha akidi."

Wafuatao, ndio wataalamu wa sheria watakaounda timu kutoka pande zote.

Afrika ya Kusini

John Dugard, mtumishi wa zamani wa Umoja wa Mataifa ndiye atakayeongoza jopo la Afrika ya Kusini.

Mbobezi wa Sheria za Kimataifa kutoka Afrika ya Kusini, Dugard ana uzoefu na ICJ, baada ya kuhudumu kama jaji wa muda mwaka 2008.

Dugard amekuwa wazi kukosoa vikali vitendo vya Israel, akisema kuwa, "Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, na baraza lake la mawaziri wanahusika na kutekeleza anachokiita uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na, pengine, uhalifu wa mauaji ya kimbari."

Wataalamu wengine wa sheria kwa upande wa Afrika Kusini ni pamoja na Wakili Mwandamizi Adila Hassam, Tembeka Ngcukaitobi, na wakili wa kimataifa Max Du Plessis.

Kikosi cha Afrika Kusini kinachoongezwa nguvu na Blinne Ni Ghralaigh kutoka Ireland na Muingereza Vaughan Lowe. Timu itawajumuisha pia wakili wengine wakiwemo Tshidiso Ramogale, Sarah Pudifin-Jones na Lerato Zikalala.

Timu ya Utetezi kutoka Israeli

Israel imemchagua wakili wa Uingereza Malcolm Shaw kuiwakilisha katika mahakama ya ICJ.

Shaw anatajwa kama mmoja ya wataalamu wa sheria za kimataifa na amewahi kutetea kesi hapo The Hague.

Muingereza huyo amejijengea jina kwa kutoa ushauri kuhusu migogoro ya kimaeneo; sheria ya bahari; haki za binadamu; kujitawala, usuluhishi wa kimataifa,” hii ni kwa mujibu wa wasifu wake uliohifadhiwa katika makabrasha ndani ya mahakama ya Essex, Kusini-Mashariki mwa Uingereza.

Kwa nyakati tofuauti, Shaw pia amehusika kutoa ushauri wa kisheria kwa nchi mbalimbali zikiwemo Uingereza, Ukraine na Serbia.

Mbali na ICJ, Shaw amewahi pia kuhusika katika kesi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, Mahakama ya Haki ya Ulaya, na Mahakama nyingine kubwa duniani.

Nguli huyo pia anatajwa kuwa mmoja wa mawakili wanne, kuiwakilisha Israeli katika vikao vya ICJ, japo majina na wasifu wa mawakili bado haujawekwa wazi.

Jopo la Waamuzi

ICJ inaundwa na majaji 15 waliochaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kwa ajili ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka tisa.

Kulingana na sheria na miongozo ya ICJ, nchi ambayo inahusika na kesi na haina Jaji katika jopo hilo, ina wajibu wa kupendekeza Jaji wa muda, kama ilivyotokea kwa Afrika ya Kusini na Israeli.

Ni kwa muktadha huo, Afrika ya Kusini imemteua Dikgang Moseneke, aliyekuwa naibu wa Jaji Mkuu nchini humo na gwiji wa masuala ya kisheria, wakati Israeli ilimchagua Aharon Barak, Rais wa zamani wa Mahakama Kuu wa nchi hiyo.

Pia alitetea uamuzi wa Israeli wa kujenga ukuta wa kujitenga kupitia Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kufuatia uamuzi wa 2004 wa ICJ kutangaza kuwa ni kinyume cha sheria.

Majaji wengine 15 wa mahakama hiyo wanatoka nchi tofauti. Joan Donoghue kutoka Marekani ndiye rais wa mahakama hiyo huku Kirill Gevorgian wa Urusi akiwa makamu wa rais.

Kutoka Afrika, jopo hilo linaundwa na Abdulqawi Yusuf kutoka Somalia, Julia Sebutinde wa Uganda na Mmorocco Mohamed Bennouna.

Majaji wengine wa ICJ ni pamoja na Xue Hangin kutoka China, Peter Tomka wa Slovakia, Mfaransa Ronny Abraham, Mbrazili Leonardo Nemer Caldeira Brant, Dalveer Bhandari wa India, Patrick Lipton Robinson wa Jamaica, Hilary Charlesworth wa Australia, Nawaf Salam wa Lebanon, Yuji Iwasawa wa Japan na Mjerumani Georg Nolte.

TRT Afrika