Naibu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua amemuomba msamaha Rais wa nchi hiyo William Ruto.
Gachagua, anayekabiliwa na sakata la kung’olewa madarakani, siku ya Oktoba 6 amesema kuwa hakuwa anajua kosa lake na kwamba ni vyema Rais William Ruto amsamehe, ikiwa amemkosea kwa njia yoyote ile.
Naibu huyo wa Rais, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa ibada ya misa katika eneo la Karen jijini Nairobi siku ya Oktoba 6, alisema kuwa hakuwa anajua anatambua makosa yake yoyote, huku akiomba apewe nafasi ya pili kuwatumikia Wakenya.
“Naomba kumwambia kaka yangu, Rais William Ruto: Kama nimekukosea katika ari yangu ya ufanyaji kazi, naomba uniwie radhi,” alisema Gachagua wakati wa ibada ya misa iliyofanyika katika eneo la Karen jijini Nairobi.
Naibu huyo wa Rais, pia alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Ruto kwa niaba ya mke wake, Dorcas Rigathi.
Gachagua pia aliwaomba msamaha Wakenya, huku akikabiliwa na sakata la muswada wa kumng’oa madarakani kiongozi huyo.
“Kwa Wakenya wote, kama kuna jambo lolote lile tulilolifanya au kulisema na likawakwaza, mnisamehe.”