Mvutano kati ya mahakama na rais wa Kenya unaendelea.  Picha: AFP

Mzozo kati ya Rais William Ruto wa Kenya na mahakama unaendela kuwa mkubwa huku pande mbili hizo zikionekana kuzozana.

Haya yanajiri baada ya Rais Ruto kutoa matamshi kuhusu idara ya mahakama ya serikali, akidai kuwa baadhi ya maamuzi yaliyotolewa na Idara ya Mahakama yanapunguza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya serikali yake.

"...Kuna maafisa wengi wazuri katika mahakama na tutang'oa wafisadi. Tutafanya hilo,,," rais Ruto amesema katika ujumbe wake kwa mtandao wa X.

Idara ya mahakama nchini humo ilimkosoa rais Ruto kutokana na matamshi yake kuwa baadhi ya majaji "wafisadi" walikuwa wakipanga njama na "makampuni" ili kukatisha tamaa serikali kupitia mfumo wa mahakama.

Wiki iliyopita, kiongozi huyo alisema baadhi ya wanasiasa wa upinzani, makundi ya watu na majaji wameungana kuzuia miradi ya utawala wake.

Baadhi ya miradi aliyoangazia ni pamoja na pendekezo la serikali la kuwepo kwa ushuru wa nyumba wa asili mia1.5 na sera mpya ya bima ya afya ambayo itapelekea asili mia 2.75 ya mishahara ya wafanyakazi kukatwa katika mpango wa matibabu unaosimamiwa na serikali.

"Mahakama yetu, tunawaheshimu, lakini kutokujali kwa maafisa wa mahakama wafisadi lazima kukomeshwe nchini Kenya... tutaikomesha, vyovyote itakavyokuwa," Ruto alisema.

"Baadhi ya watu wawili au watatu walienda mahakamani na kuwahonga majaji. Sasa mpango wetu kama serikali umepata msukosuko. Miradi ya barabara, huduma za afya kwa wote na nyumba zote zimekwama," rais aliongezea.

Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome amemkosoa rais kutokana na matamshi yake akisema kuwa iwapo ana mabishano na majaji yeyote, kuna njia za kisheria za kuwasilisha malalamiko yake.

Koome ameonya juu ya hatari ya "machafuko" ikiwa uhuru wa idara ya mahakama hautaheshimiwa.

Sasa Chama cha Wanasheria cha Kenya, (LSK) kimetangaza kuwa kitaandaa maandamano ya amani kote nchini kutetea utawala wa sheria na mshikamano na Idara ya Mahakama.

Mawakili wanadai rais anatishia demokrasia ambayo inaruhusu uhuru wa vyombo vya sheria. "Katiba inaamuru kwamba mamlaka hiyo ya rais itumike na kutekelezwa kwa kuzingatia masharti ya kikatiba," alisema.

Wanadai kuwa wanatambua mahakama kutokana na jukumu lake kama "mlinzi wa katiba" na "udhibiti dhidi ya unyanyasaji."

TRT Afrika