wanaokimbilia mikopo ya haraka na kukopa ili kutatua tatizo moja huishia kujichimbia zaidi kwenye madeni./ Picha: Reuters 

Steve Wanyoike hupokea hati yake ya malipo tarehe 26 kila mwezi. Siku chache baadaye ana uhakika mshahara wake utawekwa kwenye akaunti yake.

Kazi yake kama mhudumu katika mkahawa humlipa kiasi cha kutosha kukidhi mahitaji yake ya kila siku. Akiwa na mambo muhimu kama vile kodi ya nyumba, usafiri wake na milo yake ikiwa imepangwa, anabakiwa na kitu chochote kwa kile anachokiita anasa.

‘’Pay slip yangu ni kama kisu moyoni kila siku. Ni ukumbusho wa mara kwa mara kuwa mimi ni maskini.. haha’’ anatania.

Lakini hili si jambo la kucheka. Sio kwa Steve au mtu mwingine yeyote. Kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha huko Nairobi, wafanyakazi wengi wa kipato cha kati wanalazimika kuishi kwa kubahatisha mlo wa kila siku.

Wengi wanalalamika kwamba mishahara yao ilikuwa na thamani miaka 5 iliyopita, lakini sasa hali tofauti kabisa.

‘’Miaka 7 iliyopita, nilifanya kazi katika mkahawa ambapo nilipata mshahara wa chini hata kuliko ninachopata sasa. Lakini kwa namna fulani gharama zangu zilifikiwa na hata nilikuwa na ziada. Lakini sasa sijui pesa zangu zinakwenda wapi. Zinatoweka mara tu zinapoingia,’’ anaambia TRT Afrika.

Ingawa ni kweli uchumi umekuwa mgumu hivi karibuni, wataalam wanaonya kuwa mara nyingi tunajiingiza wenyewe katika hali ngumu na fedha zetu.

‘’Watu wengi huhitimu shule bila taarifa au maarifa kuhusu jinsi ya kusimamia fedha zao za kibinafsi,’’ anasema Charles Macharia, mshauri wa masuala ya fedha jijini Nairobi. ‘’Ni muhimu kujua mapema jinsi unavyopanga kutumia pesa zozote utakazopata.’’ Anaongeza.

Steve anasema payslip yake inakatwa madeni mengi na hilo ndilo linaloathiri bajeti yake ya kila mwezi.

‘’Payslip yangu inakatwa mkopo wa benki, sehemu moja huenda kulipa mkopo wa sacco ya ustawi pia. Na hizo ni zile tu ambazo zinakatwa moja kwa moja kwenye payslip yangu.’’

Lakini anasema japo mikopo inakuja na ubaya wake, hawezi kuishi bila mikopo hiyo.

‘’Kama serikali yenyewe inadaiwa na China, mimi ni nani niishi bila mkopo? ‘’ anacheka Steve. Njia za haraka za kutatua shida zako za kifedha mara nyingi sio bora.

Kulingana na wataalamu, watu wanaokimbilia mikopo ya haraka na kukopa ili kutatua tatizo moja huishia kujichimbia zaidi kwenye madeni.

limekuwa jambo la kawaida kwa mfano kuona benki zikiuza mikopo inayopatikana kwa urahisi katika mitaa ya Nairobi. Pia mifumo ya pesa ya simu inasukuma mikopo usoni mwako kila kukicha.

Hii inaweza kuwa baraka ikiwa unatafuta uwekezaji, lakini pia inaweza kukuongoza kwenye mtego wa madeni.

‘’Elewa Masharti ya Mkopo. Jifahamishe na viwango vya riba, ada, na masharti ya ulipaji ili kuepuka gharama zilizofichwa zisiharibu fedha zako,’’ Charles anaiambia TRT Afrika. ‘’ Muhimu ni kuhakikisha unakopa kwa mahitaji muhimu au uwekezaji wenye tija, kuepuka vishawishi vya kukopa kupita kiasi,’’ anaongeza.

Kanuni ya msingi, linapokuja suala la kukopa kutoka benki na wakopeshaji wengine ni kuepuka kukopa kwa matumizi isiyokuwa lazima sana.

Wataalamu wanashauri kuzingatia tu mikopo inayosaidia shughuli za kuzalisha mapato, kama vile ubia wa biashara au uwekezaji mwingine.

Mtego mwingine wa haraka ni wakopeshaji wasiodhibitiwa kama vile Shy Lock na wakopeshaji wa kibinafsi. Wakopeshaji hawa mara nyingi hujitokeza wakati wa dharura na kutoa masharti ambayo ni magumu ambayo wakati mwingine yanakuwa hata kinyume cha sheria.

Wakopeshaji hawa wako tayari kukukaba na malipo ya riba wanayotoza huku ukishindwa kulipa pesa asili ulizokopa.

Steve anasema, wazo la kupunguza mtindo wake wa maisha hapo kabisa, kwani anahitaji kuendelea kushika nafasi yake mbele ya macho ya watu.

‘’Ninavunjika moyo ninapotazama miaka yote ambayo nimekuwa nikifanya kazi, lakini sina cha kuonyesha,’’ anasema Steve.

Lakini tabia hii kulingana na wataalam imesababisha watu wengi katika hali mbaya, ikiwa ni pamoja na madeni makubwa, kushindwa kulipa na kufilisika.

‘’Iwapo unatatizika na deni, wasiliana na mtaalamu wa fedha kwa mwongozo, na uwasiliane na wakopeshaji ili kujadiliana upya njia ya kulipa ikiwezekana,’’ anashauri Charles. ‘’Usisahau, benki zipo kwa ajili ya kutengeneza pesa, hivyo hakikisha unazitumia kujitengenezea pesa zako mwenyewe kadri uwezavyo. Na jifunze kuishi kulingana na uwezo wako,’’ anasema Charles.

TRT Afrika