Barani Afrika kulikuwa na nchi 17 ambazo zilitakiwa kufanya uchaguzi mwaka 2024, lakini ni 13 tu ndizo zilizofanya. / Picha: AP

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mwaka wa 2024 umeitwa “super elections year” yaani mwaka wa kipekee kwa kuwa na idadi kubwa ya nchi zenye kufanya uchaguzi. Nchi nyingi duniani zilifanya Uchaguzi Mkuu wa mifumo tofauti. Hapa barani Afrika kati ya nchi 17 zilizotarajiwa kuendesha uchaguzi mwaka 2024 , ni 13 zilizoweza kufanya.

Wingu la mabadiliko lilitanda katika nchi kadhaa na kutetemesha misingi ya vyama tawala ambayo awali ilikita mizizi yake.

Kwa mfano nchini Afrika Kusini kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo kufanya uchaguzi huru wa kwanza mwaka 1994, chama tawala cha African National Congress (ANC) kilipoteza wingi wa kura katika uchaguzi mkuu Mei 2024 na chama tawala kulazimika kuungana na vyama vya upinzani kuunda serikali mseto.

"Kupoteza nguvu zetu katika uchaguzi wa 2024 kumetuma ujumbe nyumbani kwa njia ya moja kwa moja na tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa unasikika na kujibiwa ipasavyo," Katibu Mkuu wa chama cha ANC Fikile Mbalula aliwaambia wanachama wenzake.

Chama cha ANC cha Afrika Kusini chini ya Rais Cyril Rampaphosa kilishindwa kupata asilimia ya kutosha kutengeza serikali pekee yake katika uchaguzi mkuu wa Mei 2024/Picha AFP

"Kulazimishwa kufanya kazi na vyama ambavyo kwa kawaida tusingependa kuwa navyo serikalini, sio chaguo ambalo ANC ingelifanya katika mazingira tofauti. Hata hivyo, inakuwa ni jambo lisiloepukika wakati umepoteza mamlaka ya kutawala peke yako," aliongezea.

Katika nchi jirani ya Botswana, Oktoba 2024, Chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kiliongoza nchi kwa miaka 58 kilishindwa na upinzani. Rais Mokgweetsi Masisi akapeana urais kwa Duma Boko wa Umbrella for Democratic Change (UDC).

“Sithubutu kushindwa. Sithubutu kukata tamaa,” rais Boko alisema katika hotuba yake ya kwanza baada ya ushindi, akiadihi kurejesha imani ya watu kwa serikali na kuhakisha uchumi wa Botswana inayojulikana na uzalishaji wa almasi, unanawiri tena.

Duma Boko wa chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC) ndiye Rais wa sasa wa Botswana/ Picha: Reuters

Disemba 2024 raia wa Ghana walimrudisha madarakani rais wao wa zamani John Dramani Mahama, ambaye hapo awali alihudumu kwa muhula mmoja tu. Chama tawala cha New Patriotic Party (NPP) ambacho makamu wa rais wa nchi hiyo Mahamudu Bawumia ambae ndie aliyekuwa akitafuta urais, kilishindwa.

"Kura zote za maoni zinaonyesha kuwa uchumi na ukosefu wa ajira ni masuala muhimu na ndiyo sababu kampeni yetu iliyaangazia hayo."

John Mahama aliwahi kuwa rais wa Ghana kati ya 2012 na 2017. Hapo baadaye Rais anayeondoka madarakani Nana Akufo-Addo alichukua hatamu kutoka 2017 na kuhudumu kwa mihula miwili.

John Mahama aliwahi kuwa rais wa Ghana kati ya 2012 na 2017 picha: Reuters 

Viongozi wapya

Nchini Senegal, Uchaguzi uliokuwa umepangwa Februari 2024 uliahirishwa na aliyekuwa rais wakati huo Macky Sall, wiki chache tu kabla ya tarehe iliyopangwa kufanyika, hali iliyozua machafuko nchini.

Macky Sall baadaye alijiuzulu na Novemba 2024 chama tawala cha Pastef kilirudi madarakani baada ya kushinda muungano wa vyama vya upinzani ambao Sall alikuwa anaongoza.

Nchini Senegal Chama tawala cha Pastef kilirudi madarakani kwa uongozi wa Bassirou Diomaye Faye / Picha: Getty 

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye sasa ndiye kiongozi mwenye umri mdogo zaidi aliyechaguliwa kupitia uchaguzi Afrika.

Mei 2024 Chad ilimtangaza Mahamat Idriss Deby kama mshindi kwa uchaguzi mkuu. Deby ni mwanajeshi ambaye alijitangaza kiongozi wa mpito wa Chad baada ya baba yake Idriss Deby kuuawa 2021.

Mahamat Idriss Deby rais wa sasa wa Chad ni mwanajeshi ambaye alijitangaza kiongozi wa mpito wa Chad baada ya baba yake Idriss Deby kuuawa 2021/ picha: AFP

Nchini Mauritius chama tawala L’Alliance Lepep kiliondolewa baada ya chama cha upinzani, Alliance of Change (ADC) kinachoongozwa na Navin Ramgoolam kunyakua kura mingi za bunge dhidi na kumtuma nyumbani aliyekuwa rais wao Pravind Jugnauth.

Marais waliobaki

Na kuna zile nchi ambazo marais waliokuwepo waliendeleza uongozi wao.

Nchini Comoros Rais Azali Assoumani alichaguliwa kwa muhula wake wa nne.

Azali Assoumani ni afisa wa zamani wa kijeshi ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi mwaka wa 1999 na kushinda uchaguzi wake wa kwanza mwaka wa 2002/ picha: AFP

Julal 2024 nchini Rwanda Rais Paul Kagame alirudi tena kuhudumua kwa awamu yake ya nne baada ya kushinda kwa zaidi ya 99% ya kura .

Mipango ya uchaguzi yagonga mwamba

Septemba 2024, Sudan Kusini ambayo ipo chini ya serikali ya mpito tangu 2018 iliahirisha uchaguzi wake mkuu wa kwanza uliopangwa kufanyika Disemba 2024 hadi Disemba 2026, ikidai kuwa haikuwa tayari.

"Ofisi ya Rais, chini ya uenyekiti wa Rais Salva Kiir Mayardit, imetangaza kuongeza muda wa kipindi cha mpito kwa miaka miwili na kuahirisha uchaguzi, ambao awali ulipangwa kufanyika Disemba 2024 hadi Disemba 22, 2026," ofisi ya Rais Kiir ilisema.

Rais Salva Kiir na aliyekuwa mpinzani wake Riek Machar wanaongoza Sudan Kusini kwa mfumo wa serikali ya mpito/ Picha: wengine 

Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa zamani aliyegeuka kuwa naibu, Riek Machar, walitia saini makubaliano ya amani mwaka 2018 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kusababisha vifo ya takriban watu 400,000.

Burkina Faso ambayo iko chini ya uongozi wa kijeshi ilitarajiwa kufanya uchaguzi Julai 2024 ili wanajeshi wapitishe uongozi kwa wananchi .

Kiongozi wa Kijeshi nchini Burkna Faso amesema usalama ni muhimu kwanza kabla ya uchaguzi/ Picha: Reuters 

Lakini mpango huu uligonga mwamba baada ya kiongozi wa kijeshi Kapteni Ibrahim Traore kuongeza muda wa uongozi wa kijeshi kwa miaka mitano kutoka Julai 2024.

Nchini Mali wanajeshi ambao wanaongoza nchi hiyo waliahidi 2022 kufanya uchaguzi baada ya miaka miwili.

Lakini Februari 2024 ilipotarajiwa hawakutimiza ahadi hii.

Uchaguzi wa utata

Na tunapofunga pazia la mwaka 2024, wananchi wa Msumbiji bado hawajakubali matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwakani.

Upande wa upinzani nchini Msumbiji umekataa ushindi wa chama tawala cha FRELIMO / Picha: Reuters 

Ushindi wa chama tawala cha FRELIMO chini ya Daniel Chapo, ulipotangwazwa kwa asilimia 70.7% ya kura, hata hivyo, upinzani umeyakataa matokeo hayo na kusababisha machafuko tangua wakati huo.

Huku jirani yao Namibia wamepata Rais wa kwanza mwanamke, Netumbo Nandi-Ndaitwah baada ya chama tawala cha SWAPO kushinda uchaguzi mkuu, Novemba 2024.

Kufuatia kifo cha Rais wa Namibia Geingob mnamo Februari 2024, Nandi-Ndaitwah aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais./ Picjha: Wengine 

Kufuatia kifo cha Rais wa Namibia Geingob mnamo Februari 2024, Nandi-Ndaitwah aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais, akimrithi Nangolo Mbumba ambaye aliteuliwa kuwa Rais wa mpito hadi uchaguzi mkuu wa Novemba 2024. Mbumba hakutaka kugombea urais na hapo Nandi akasimama kwa tiketi ya chama tawala.

TRT Afrika