Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Februari 18, 2024 sanamu la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere lilizinduliwa katika makao makuu ya Tume ya Umoja wa Afrika, AUC, mjini Addis Ababa Ethiopia.
Sanamu la Nyerere limesimama pamoja na sanamu za viongozi wengine mashuhuri wa Kiafrika, kama Haile Selassie wa Ethiopia na Kwame Nkurumah wa Ghana. Sanamu yake katika uwanja wa AUC ni ishara ya mchango wake katika mapambano ya uhuru wa bara hili.
Nyerere alikuwa mmoja wa waasisi wa Muungano wa Umoja wa Afrika, OAU mwaka 1963 ambao lengo kuu lilikuwa ni kuondoa ukoloni barani Afrika.
"Bara letu ni moja, na sisi sote ni Waafrika. Shirika hili linaashiria dhamira yetu ya kusonga mbele pamoja," Julius Nyerere alisema katika mkutano wa uzinduzi wa Umoja wa Umoja wa Afrika mwaka 1963.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC, Moussa Faki Mahamat alisema kupitia Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilikuwa msingi wa mapambano ya Ukombozi wa Afrika.
“Chini ya uongozi wake, Tanzania imekuwa kimbilio la harakati za ukombozi katika bara zima. Umoja wa Kamati ya Ukombozi wa Muungano wa Umoja wa Afrika ulipata makao yake makuu nchini Tanzania hadi kuvunjwa kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini mwaka 1994,” Faki alisema.
Maneno ambayo Nyerere aliyasema tarehe 22 Oktoba 1959 yameandikwa kwenye sanamu hiyo iliyo katika makao makuu ya tume ya AU:
"Tungependa kuwasha mshumaa na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ambao ungeangaza nje ya mipaka yetu na kutoa matumaini pale ambapo kulikuwa na kukata tamaa, upendo ambapo kulikuwa na chuki na utu ambapo kabla ya hapo kulikuwa na unyonge tu."
Mapambano ya kupinga ukoloni katika bara hili yalipata nguvu nchini Tanzania chini ya Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru mwaka 1961 na baadae Rais wa kwanza wa nchi mpya ya Tanzania 1964.
Viongozi ambao Nyerere aliungana nao katika ajenda ya uhuru wa bara ni pamoja na chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini na Pan African Congress (PAC) cha Afrika Kusini, FRELIMO kilipotaka kupindua utawala wa Ureno nchini Msumbiji, na ZANLA (yaa Robert Mugabe) katika mapambano yake ya kuung'oa utawala wa Wazungu nchini Zimbabwe (iliyokuwa Rhodesia).
Kuanzia katikati ya miaka ya 1970, Nyerere alikuwa sehemu ya " front Line States" yaani 'Nchi Zilizokua Mstari wa Mbele.'
Haya yalikuwa ni mataifa ambayo yalitoa msaada katika kampeni ya kuuondoa ukoloni nchini Afrika Kusini.
Pia walimjumuisha Samora Moises Machel wa Msumbiji, Quett Masire wa Botswana, Eduardo dos Santos kutoka Angola na Kenneth Kaunda wa Zambia.
Nyerere alikuwa mmoja wa viongozi tisa walioungana mwaka 1980 kuanzisha Kongamano la Uratibu wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC), ambalo baadaye lilikuja kuwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Lengo lake ni kukuza umoja wa kiuchumi, kisiasa na kijamii katika eneo la Kusini mwa Afrika,
Nyerere na Uganda
Katika ukanda wa Afrika Mashariki hamu ya Nyerere ya umoja wa kikanda ilikuwa wazi.
“Mwalimu Nyerere, alijitolea kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili Uganda na Kenya ziwe huru kwa wakati mmoja na kuwa nchi moja. Lilikuwa kosa kutopokea wazo hili. Afrika inaweza kuwa Amerika ya Kusini barani Afrika badala ya kuwa Umoja wa Afrika barani Afrika,” Museveni alisema katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma alipoadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 80 mnamo 2024.
Uganda ina uhusiano wa karibu na Nyerere.
Kwa heshima ya mchango wake katika mapambano ya ukombozi barani Afrika Rais Yoweri Museveni alizindua Kituo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala ambako Nyerere alisoma.
Kilizinduliwa mwaka wa 2018 na kilianzishwa kwa ajili ya mazungumzo kati ya vizazi kuhusu historia ya Afrika, utafiti wa harakati za mapinduzi ya Afrika, na kama kituo cha ujuzi na utafiti.
Serikali ya Uganda ilitenga (zaidi ya dola 620,000) Shilingi bilioni 2.3 kwa mradi huo kuelekea ujenzi wa muundo mpya katika kampasi ambapo kiongozi huyo wa Tanzania alikaribishwa akiwa mwanafunzi.
Baada ya elimu yake ya sekondari, Nyerere aliendelea na masomo yake kupitia ufadhili katika Chuo cha Makerere.
Katika taasisi hiyo ya serikali alisoma kozi ya ualimu kati ya 1943 hadi 1947.
“Mimi ni wa urithi wa upinzani na uliongozwa na Mwalimu Nyerere. Unapaswa kusoma kwa kina kile Mwalimu alichosimamia na kujua vipengele vipya vinavyoweza kuongezwa. Huwezi kumzungumzia bila kuzungumza kuhusu Afrika,” Rais Museveni aliwaambia wanafunzi katika Chuo Kikuu hicho.
Nyerere baadaye angekuwa jambo muhimu sana kwa historia ya kisiasa ya Uganda, Oktoba 1978 Uganda chini ya rais wake Jenerali Iddi Amin Dada ilijaribu kunyakua sehemu ya Tanzania.
Aliivamia Kagera kaskazini mwa Tanzania na mwezi mmoja baadaye Amin akatangaza kuwa ametwaa ardhi yote ya Tanzania kaskazini mwa Mto Kagera.
Mwaka 1979, Julius Nyerere aliiongoza Tanzania katika vita dhidi ya Uganda, na kusababisha waliomuunga mkono Amin Dada kufukuzwa katika ardhi ya Tanzania. Baadaye akaivamia Uganda na kuupindua utawala wa Amin.
Safari ya Nyerere katika Bara la Amani
Mnamo 1993 Burundi ilitupwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya mauaji ya rais wa kwanza wa Kihutu aliyechaguliwa kidemokrasia na wanajeshi wa Kitutsi.
Miaka miwili baadaye Nyerere alianza mchakato wa amani kati ya makundi yanayopigana.
Miaka kadhaa baadaye baada ya kuwezesha mazungumzo ya Nyerere na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela, Agosti 2000 vyama hivyo vilitia saini makubaliano ya Amani na Maridhiano ya Arusha, au Makubaliano ya Arusha, na hivyo kumaliza miaka 12 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hii ilikuwa ni moja tu ya juhudi za kuituliza Afrika ambazo hayati rais wa Tanzania anakumbukwa nazo.
Katika makao Makuu ya Tume ya Umoja wa Afrika kazi za amani za Mwalimu Julius Nyerere zinathaminiwa na ukweli kwamba Idara ya Amani na Usalama ya Tume ya AU inakaa katika jengo lililopewa jina lake, 'Jengo la Amani na Usalama la Julius Nyerere' lililozinduliwa mwaka 2016.
Julius Kambarage Nyerere alikufa katika hospitali ya London baada ya kuugua saratani ya damu mnamo Oktoba 14, 1999.
Lakini bado mchango wake barani Afrika unabaki kuwa kumbukumbuya kipekee ya kihistoria.