Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Ni miaka 28 sasa tangu ajali ya meli ya Mv Bukoba itokee nchini Tanzania.
Lakini kwa Godwin Shinyanga, tukio hilo ni kama limetokea jana tu.
“Bado kumbukumbu hazijafutika kichwani mwangu, bado nimebakiwa na maumivu makubwa,” anakumbuka Shinyanga, wakati wa mahojiano yake maalumu na TRT Afrika.
Mtumishi huyo wa umma alimpoteza mama yake, Ritha Justus na mdogo wake anayemfuatia Evelyine, ambaye alikuwa na umri wa miaka sita tu, wakati ajali hiyo inatokea.
Kinachomuumiza zaidi hadi leo ni miili ya wapendwa wake hao kutopatikana baada ya siku tatu za utafutaji majini, na hivyo kuilazimu familia yake kuzika magome mawili ya miti ziwani, kama ishara ya kuwakumbuka wapendwa wao.
Shinyanga anafafanua kuwa pengine, na yeye angekuwa ni sehemu ya waathirika wa ajali hiyo ambayo iliua zaidi ya watu 800 katika Ziwa Victoria, hatua iliyomlazimu Rais wa Tanzania wa wakati huo Benjamin Mkapa kutangaza siku tatu za maombolezo, huku watumishi wa serikali wakichukuliwa hatua, kufuatia tukio hilo.
Kwa mujibu wa Shinyanga, ambaye alikuwa anasoma kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Magu, mkoani Mwanza, yeye alikuwa ni sehemu ya wanakwaya 32, waliokuwa waende Bukoba kwenye ziara ya Uinjilishaji, Mei 20, 1996.
“Nilikuwa naimba sauti ya tatu na nilikuwa napiga gitaa kwenye kwaya ya Imani kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambayo pia marehemu mama yangu alikuwa anaiimbia,” Shinyanga anakumbuka.
Kusomea bwenini
Hata hivyo, isingekuwa rahisi kwa Shinyanga kuambatana na kwaya yake pamoja na familia yake kwani alikuwa anaishi bwenini na ilikuwa ni siku ya masomo.
Licha ya kufanya mazoezi ya mwisho pamoja na kwaya hiyo, Shinyanga hakuweza kuwa sehemu ya safari hiyo ya uinjilishaji Bukoba, bila kujua kuwa ndio ingekuwa mara yake ya mwisho kuonana na mama yake na mdogo wake.
“Waliondoka siku ya Jumatano na walifanikiwa kufika salama Bukoba na kufanya huduma ya uimbaji,” anasimulia.
Safari yao ya kurudi Mwanza, ilianza jioni ya Mei 20, 2024.
Shinyanga anasema kuwa taarifa za kuzama kwa meli ya Mv Bukoba zilianza kuenea kwa kasi shuleni kwake Magu Sekondari, hali iliyoamsha wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake.
“Niliwasikia wanafunzi wenzangu wakisema kuwa kuna ajali kubwa imetokea Ziwa Victoria, hofu kubwa ilinijaa moyoni mwangu kwani ilikuwa ndio siku yao ya kurudi.
Hofu ilizidi kumjaa Shinyanga, ambaye alikuwa na miaka 16 wakati huo, baada ya kuona gari imekuja kumfuata shuleni.
“Nilihisi ubaridi mwilini mwangu, nikajua lazima kuna taarifa mbaya nitakazosikia.”
Ajali yenyewe
Meli ya Mv Bukoba, ikiwa na abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 ilizama majini kwenye Ziwa Victoria mwambao wa Bwiru Jijini Mwanza, takribani kilomita 30 kabla ya kufika nchi kavu.
Tukio hilo, lilitokea nyakati za asubuhi, wakati wengi wa abiria wakiwa wanajiandaa kusafisha vinywa vyao.
Kulingana na simulizi za baadhi ya wanakwaya walionusurika kwenye ajali hiyo, mama mzazi wa Shinyanga aliamua kubaki na Evelyine sehemu ya chini ya meli, kutokana na hali ya baridi na upepo mkali kutoka ziwani.
“Wengi wao waliamua kupanda upande wa juu ya meli kwenda kupiga mswaki na kufurahia mandhari nzuri ya jiji la Mwanza iliyoanza kuonekana asubuhi hiyo, kabla meli haijaanza kuyumba na hatimaye kuzama,” anaeleza.
Siku tatu za utafutaji wa miili
Iliwachukua familia ya Shinyanga siku tatu za kutafuta miili ya wapendwa wao bila mafanikio yoyote.
“Si kwenye bandari ya Mwanza wala uwanjani Nyamagana ambako tuliweza kuwaona, niliumia moyo zaidi baada ya zoezi la kutambua miili lilipozitishwa na mamlaka husika,” anakumbuka.
Ili wasipoteze kabisa kumbukumbu ya wapendwa wao, familia ya Shinyanga iliamua kuzika magome ya miti kama ishara, katika eneo la Kamanga, pembezoni mwa ziwa hilo kubwa Afrika Mashariki, kama ishara.
Tukio kama hilo pia lilifanyika Bukoba, mahali anapotoka marehemu mama yake.
Kuwakumbuka
Mwaka huu, Shinyanga amepanga kwenda kufanya ibada katika eneo la Igoma, ambapo kumejengwa mnara maalumu wenye majina ya wale wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
“Jina la mama yangu na la mdogo wangu yako pale, itakuwa siku muhimu na ya tafakari kubwa sana katika maisha yangu,” anaiambia TRT Afrika.
Miaka 28 baadae, Shinyanga bado anawakumbuka sana marehemu mama yake pamoja na mdogo wake.
“Mama yangu alikuwa mtu muhimu sana maishani mwangu, alitaka nifanikiwe maishani, ninatamani angekuwepo anione nilipo leo,” anasema.
Kwa upande wa Evelyine, japo alifariki akiwa na umri wa miaka sita tu, Shinyanga anakumbuka namna walivyofanana sana kwa sura.
“Ningetamani sana tukue pamoja, bado namkumbuka sana Evelyine.”
Flaviana Matata sio jina geni katika ulimwengu wa uanamitindo.
Mwanamitindo huyo, pia alipompoteza mama yake kwenye ajali ya Mv Bukoba.
Imekuwa ni desturi yake, kila mwaka kutembelea makaburi ya waathirika yaliyoko katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza.
Kupitia taasisi yake ya Flaviana Matata Foundation, mwanamitindo huyo amekuwa akitoa misaada ya vifaa vya uokozi kwa mamlaka zinazosimamia usafiri wa majini mkoani Mwanza, kama ishara ya kumkumbuka mpendwa wake.
Umbali mchache kabla ya kufika Mwanza
Meli hiyo ilizama baada ya kuzidiwa na uzito wa abiria pamoja na mizigo, kulingana na ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo.
MV Bukoba ilizinduliwa mwaka 1979 na Rais wa kwanza wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere, ilidumu kwa miaka 17 tu, na kupinduka ikiwa katika safari zake za kawaida, ikitokea katika bandari ya Bukoba kupitia Kemondo.
Ilizama ikiwa imebakisha umbali wa maili moja na nusu ili iweze kutia nanga katika bandari ya Mwanza Kaskazini, hali ambayo ilikwishawapa abiria matumaini ya kufika salama kwa abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.
Ilikuwa tayari iko jirani kabisa na ufukwe wa Shule ya Sekondari Bwiru, ambako sasa kumejengwa mnara wa kumbukumbu ya wahanga wa ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea katika Ziwa Victoria. Ukosefu wa vifaa vya kuokolea majini ulikuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa vifo vya abiria, waokoaji wa ajali hiyo walisubiriwa kufika nchini kutokea Afrika Kusini, ambao waliweza kuogelea na kuokoa baadhi ya maiti chache zilizokuwa zimezama umbali wa mita 25 chini ya maji.
Ajali hiyo imebaki kuwa kumbukumbu mbaya kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na mikoa jirani na Watanzania kiujumla. Kila mwaka ifikapo Mei 21, Tanzania hukumbuka kwa kuomboleza vifo vya abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.
Baadhi yao miili yao haikupatikana na kusababisha maziko yao kufanyika humo humo majini huku meli hiyo ikigeuzwa kuwa kaburi lao la pamoja.
Makaburi ya wahanga wengine yapo katika Kitongoji cha Igoma umbali wa kilometa nane kutoka katikati ya Jiji la Mwanza.
Hadi sasa hakuna sababu rasmi zilizokwishatolewa na Serikali kuhusu chanzo cha ajali ya MV Bukoba ingawa wapo baadhi ya watu na viongozi wanaosema ilitokana na meli hiyo kujaza abiria na mizigo kupita kiasi, na kwamba ilikumbwa na dhoruba kali ziwani.
Meli hiyo ambayo ilijengwa na kampuni ya Kibelgiji, tangu kuzinduliwa kwake ilikuwa na tatizo la uwiano.
Kutokana na ajali hiyo, Tanzania iliunda iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya ajali ikiwa na lengo la kufanya ukaguzi kwa vyombo vyote vya usafiri wa majini na nchi kavu.