Kiongozi huyo wa zamani wa IEBC alikuwa amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi ambapo alikuwa kwa matibabu kwa takriban wiki moja. Chebukati aliyekuwa na umri wa miaka 63, alifariki siku ya Alhamisi jioni.
Inasemekana kuwa kiongozi huyo wa zamani wa tume ya IEBC alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo. Bado haijabainika alikuwa anaugua ugonjwa gani.
Huduma ya Chebukati
Chebukati alihudumu kama mwenyekiti wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita na alistaafu Januari 2023. Aliongoza Uchaguzi Mkuu wa 2017 na 2022 nchini Kenya. Alikuwa wakili mwenye uzoefu wa miaka 37 na aliendeleza shughuli zake binafsi za uanasheria kwa miaka 20.
Aliwahi kuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga. Hata hivyo alijiuzulu, kabla ya kuomba nafasi ya Uenyekiti wa tume huru ya uchaguzi.
Chebukati ameacha mjane,Mary Chebukati aliyepata naye watoto kadhaa.