Muswada mpya ulio bungeni nchini Kenya, unalenga usajili wa wakulima wote wa mazao ya mboga mboga - wadogo kwa wakubwa.
Iwapo utapitishwa, wakulima wa mazao ya mboga mboga watahitajika kutumia vifaa vya kilimo kutoka kwenye chanzo kilichosajiliwa.
Hii itajumuisha wanaozalisha hasa maua, matunda, mboga mboga, mimea ya mapambo, na mimea ya dawa.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Mazao ya Mimea ya 2024, unasema kuwa mtu sharti awe na leseni ili aweze kusindika, kuagiza nje au kuuza nje bidhaa za mboga mboga.
Wafanyabiashara hao pia watalazimika kujisajili na serikali za kaunti zinazosimamia shughuli zao - bila malipo.
Wauzaji nje na waagizaji wangetakiwa kupata leseni kutoka serikalini ili kushughulikia mazao mbalimbali. Wakiukaji wanaweza kutozwa faini ya kati ya shilingi milioni moja hadi milioni mbili au kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu.
"Mtu hataruhusiwa kuweka mazao yake kwa biashara ya ndani ya nchi isipokuwa kama amepewa leseni na serikali ya kaunti husika," muswada huo unasema.
Muswada huo pia unalenga kuanzisha ushuru wa mazao ya bustani kwa mauzo ya nje na uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Ushuru wa mauzo ya nje utatozwa asilimia 1.5 kwa mazao au bidhaa yoyote ya mboga mboga.
Mazao yaliyowekwa kwenye makopo, chupa za kuhifadhia yaliyokaushwa au yale yanayoletwa viwandani kwa ajili ya kuhifadhiwa katika makopo au chupa hayatalipishwa ushuru.
Bidhaa za mboga mboga zilizoagizwa kutoka nje ya nchi zitatozwa 4% ya ushuru.
Sheria inapendekezwa kutozwa 2% ya thamani ya mazao ya bustani yaliyoagizwa kama mazao mapya.
"Mtu ambaye atashindwa kulipa ushuru wa mazao ya bustani uliyowekwa chini ya Sheria hii atakuwa na hatia," muswada huo unasomeka.
Umefafanua kwamba, serikali ya kaunti inaweza kuweka punguzo kwa maendeleo ya mazao ya mboga mboga na udhibiti wa miundombinu ya soko la mazao haya.
Iwapo wabunge watapitisha sheria hiyo, itakuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kufunga, kusindika au kuhifadhi mazao ya mboga mboga na bidhaa katika majengo yasiyo na leseni.
Mamlaka na serikali za kaunti zitakuwa na jukumu la usajili na utoaji leseni na kutoza ada.
Sheria zinaathiri biashara ya tufaha, parachichi, ndizi, shelisheli, machungwa, zabibu, mapera, shokishoki, maembe, tikiti, pichi, mananasi, matunda ya damu, komamanga, tikiti maji, mimea ya dawa, mboga, mimea ya viungo, pamoja na maua.