Kiongozi wa upinzani nchini Msumbiji, Venancio Mondlane, siku ya Jumatano ameitisha maandamano ya wiki nzima kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika Oktoba 9.
Hali ya mvutano imetawala nchi hiyo ambayo imekuwa chini ya utawala chama cha Frelimo kwa miaka 49.
Mondlane, anayeungwa mkono na chama chama Podemos, ameitisha maandamano hayo kuanzia Oktoba 31 hadi Novemba 7.
'Maandamano ya wazi'
"Tunategemea kuanza maandamano ya wazi kwa muda wa wiki nzima," alisema Mondlane kwenye mjadala mtandaoni siku ya Jumanne.
Polisi nchini Msumbiji wanasema kuwa wanaendelea kumchunguza Mondlane baada ya kuandaa maandamano ya wiki iliyopita, huku akiwa hajulikani alipo hadi sasa.
"Jeshi la polisi limefungua kesi ya jinai dhidi ya Venancio Mondlane na wafuasi wake kwa vitendo vya uwashaji moto na umiliki wa silaha," msemaji wa jeshi hilo Orlando Mudumane aliwaambia waandishi wa habari.
Matumizi ya mitandao ya jamii kwa mawasiliano
Mondlane amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuwasiliana na wafuasi wake, huku wakati mwingine hali hiyo ikikumbwa na changamoto ya kupotea kwa huduma ya mtandao nchini humo.
Kulingana na tume ya uchaguzi ya Msumbiji, Daniel Chapo kutoka chama cha Frelimo alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 71 ya kura huku Mondlane akipata asilimia 20.
Hatua hiyo, ilikilazimu chama cha Podemos, kwenda kwenye mahakama ya katiba nchini humo wakitaka kuhesabiwa upya kwa kura.
Kulingana na taasisi ya utetezi ya CIP, vyama vya upinzani nchini humo vinapendekeza mpango wa kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa.
Watu 11 wapoteza maisha katika maandamano
"Nia ni kuunganisha upinzani ila kupinga matokeo ya uchaguzi huo," ilisema taasisi hiyo kupitia taarifa yake.
Watu wapatao 11, wamepoteza maisha yao kutokana na vurugu baada ya uchaguzi, na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa, kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch.
Hata hivyo, bado haijajulikana kama wito wa Mondlane utaungwa mkono kwa kuitisha maandamano hayo.
Dosari za uchaguzi
Waziri wa Msumbiji Pascoal Ronda aliwaambia waandishi wa habari kuwa "hakuna kinachoweza kutatuliwa kupitia vitendo vya vurugu."
"Vikosi vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza dhamira yao (ya kuhakikisha) huduma za usafiri zinaendelea kama kawaida," alisema Ronda.
Waangalizi wa uchaguzi, wakiwemo kutoka Umoja wa Ulaya, wamebaini dosari kubwa kabla, wakati na baada ya upigaji kura.