Kenya itasonga mbele na mipango ya kuongoza ujumbe wa usalama ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa kwenda Haiti, licha ya mahakama mjini Nairobi wiki iliyopita kuzuia kutumwa kwa wanajeshi hao, Rais wa Kenya William Ruto aliambia Reuters Jumanne.
Kikosi hicho cha kimataifa kinalenga kukabiliana na machafuko ya magenge yaliyokithiri katika taifa hilo la Karibean, ambayo yaliua karibu watu 5,000 mwaka jana, na kinatarajiwa kufadhiliwa na Marekani.
Ujumbe huo ulitiliwa shaka baada ya mahakama ya Kenya kuamua kuwa itakuwa kinyume na katiba kupeleka maafisa nje ya nchi isipokuwa kungekuwa na "mpango wa kuafikiana" na serikali mwenyeji.
Ruto alisema Haiti iliomba usaidizi miezi kadhaa iliyopita, na alitarajia ombi litakuja hivi karibuni ambalo lingekidhi matakwa ya mahakama.
"Kwa hiyo ujumbe huo uendelee mara tu stakabadhi zote zitafanyiwa kazi kati ya Kenya na Haiti kufuatia pendekezo la mahakama ," Ruto alisema katika mkutano wa kilele wa Italia na Afrika mjini Roma.
Alipoulizwa kama majadiliano yanaendelea na Haiti kupata ombi hilo muhimu, Ruto alisema: "Hakika. Haiti wameandika rasmi, sio leo, miezi kadhaa iliyopita."
Haiti iliomba msaada kwa mara ya kwanza mwaka wa 2022 huku ghasia za magenge zikiongezeka lakini haikuweza kupata mtu yeyote aliye tayari kuchukua jukumu, huku serikali nyingi za kigeni zikiwa na wasiwasi wa kuunga mkono utawala wa nchi hiyo ambao haukuchaguliwa.
Kenya, ambayo ina historia ndefu ya kushiriki katika oparesheni za kimataifa za kulinda amani, ilijitolea Julai iliyopita na kuahidi kutuma maafisa wa polisi 1,000, ikisema inafanya hivyo kwa mshikamano na taifa ndugu.
Misheni 'inaendelea'
Bahamas, Antigua na Barbuda, na Jamaica baadaye zilisema ziko tayari kusaidia, huku Marekani ikiahidi dola milioni 200 ili kufikisha kikosi hicho kazini.
"Misheni inaendelea. Misheni hiyo ni wito mkubwa zaidi kwa ubinadamu," Ruto alisema, akisisitiza kuwa ni polisi badala ya operesheni ya kijeshi.
Umoja wa Mataifa ulisema wiki iliyopita kwamba ulirekodi watu 4,789 waliouawa na ghasia za magenge nchini Haiti mwaka jana, ongezeko la 119% kutoka 2022, na kwamba watu wengine 3,000 wametekwa nyara.