Mgombea wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane ambaye anadai kushinda uchaguzi, aliitisha maandamano. / Picha: AFP

Mgombea wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane amesema Jumatatu anafikiria kusitisha maandamano kwa siku tano ili kuruhusu mashirika ya kimataifa kuingia kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Msumbiji imekumbwa na maandamano ya ghasia ya wiki kadhaa tangu mwishoni mwa Oktoba, wakati mamlaka ya uchaguzi ilipomtangaza Daniel Chapo mwenye umri wa miaka 47 wa chama tawala cha FRELIMO kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa asilimia 71 ya kura, na kumshinda mgombea wa upinzani Venancio Mondlane aliyepata asilimia 20.

Mondlane, ambaye anadai kushinda uchaguzi, aliitisha maandamano.

Baraza la Katiba lilipewa jukumu la kusimamia kesi hiyo, na wiki iliyopita lilithibitisha ushindi wa Chapo lakini ikapunguza asilimia ya ushindi wake hadi 65%.

Hii ilisababisha maandamano mapya na yenye vurugu zaidi.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa nchini Msumbiji, Mondlane atatangaza awamu inayofuata ya maandamano mapya katika siku zijazo.

Wakati huo huo, Afrika Kusini imesema katika taarifa yake kuwa imeongeza ulinzi na doria katika mpaka wake na Msumbiji ili kuzuia na kupambana na uhalifu nyemelezi unaoweza kujitokeza kutokana na maandamano yanayoendelea katika nchi hiyo jirani.

"Serikali ya Afrika Kusini inashiriki kikamilifu na serikali ya Msumbiji katika ngazi ya nchi mbili ili kuchunguza matatizo haya na kutafuta ufumbuzi endelevu," Muundo wa Kitaifa wa Operesheni na Ujasusi wa Afrika Kusini (NATJOINTS) ulisema Jumapili.

Muungano huo umesema mataifa yote mawili yanaimarisha uhusiano wao wa kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa hatua zinazofaa zinatekelezwa ili kurejesha utulivu na kuimarisha usalama katika maeneo yaliyoathirika.

Takriban watu 277 wamefariki dunia tangu maandamano hayo yaanze nchini humo, huku vifo vingi vikisababishwa na milio ya risasi kutoka kwa maafisa wa usalama, kulingana na kundi la waangalizi wa uchaguzi wa eneo la Plataforma DECIDE.

TRT Afrika