Theluji katika Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania.Picha Reuters 

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mlima Kilimanjaro, ambao uko nchini Tanzania ndio mrefu zaidi barani Afrika. Mlima huu unakadiriwa kuwa na urefu wa zaidi ya mita 5895 kutoka usawa wa bahari.

Inasemekana kuwa mlima mkubwa zaidi duniani unaojisimamia, yaani sio sehemu ya safu ya mlima. Unajumuisha vilele vitatu vyenye asili ya volkano ambayo ni, Kibo, Mawenzi na Shira.

Watu wanaupanda mlima huu kwa sababu zao tofauti / Picha Wengine 

Kibo ndio mrefu zaidi kati ya hizo tatu na ndipo palipo na kilele cha Uhuru, kilele cha juu zaidi cha mlima huu.

Licha ya mlima huu kuwa Tanzania, lakini pia unaweza kuonekana kwa urahisi na uzuri kabisa kutoka upande wa Kenya, na baadhi ya mbuga za Kitaifa za Kenya ikijumuisha mbuga ya kitaifa ya Amboseli na Tsavo Magharibi.

Hivyo baadhi ya makampuni ya utalii nchini Kenya hutumia nafasi hiyo kuuza utalii wao wakihusisha mlima Kilimanjaro.

Kuna njia saba rasmi za kufikia kilele cha mlima Kilimanjaro/ Picha: TRT Afrika 

Mwaka 1987, Mlima Kilimanjaro uliorodheshwa na UNESCO kuwa Urithi wa Dunia kwa sababu ya uzuri wake wa asili. Kuupanda mlima Kilimanjaro kunahitaji maandalizi ya kutosha kiakili na kimwili.

Kuna njia saba rasmi za kufikia kilele cha mlima na inaweza kuchuku kati ya siku 5 hadi 10 kukamilisha safari ya kileleni. Kawaida, gharama zake ni kati ya dola za kimarekani 2000 na 3000, ikijumuisha gharama ya kila kitu.

Utahijitaji muogozaji mkuu utakayemlipa kati ya dola 20 na 25 kwa siku na msaidizi wake utampa kati ya $15 na $20 kwa siku. Mpishi wako utamlipa kama $15 kwa siku na mbeba mzigo angalau $10 kwa siku.

Kibo ndio mrefu zaidi kati ya hizo tatu na ndipo palipo na kilele cha Uhuru, kilele cha juu zaidi cha mlima huu/ picha: TRT Afrika

Kila mbeba mizigo anaweza kubeba kilo 20 tu za mzigo wako ikiwa una zaidi utahitaji kuajiri zaidi ya mmoja.

Lakini mbali na wanaotoa huduma kwa wanaopanda mlima, kuna watoa huduma wengine kama mahoteli, makampuni ya usafiri, makampuni ya ndege, wote hawa mapato yao yanatokana na mlima Kilimanjaro.

Miezi ya kupanda mlima huu ni kati ya Disemba na Machi, halafu tena kuanzia Juni hadi Oktoba.

Hii ndiyo misimu ambayo hakuna mvua, hivyo barabara zinapitika kirahisi. Safari yako itaanzia katika msitu wa Zumaridi unaokaliwa na swala, sokwe, nyati na chui, halafu itakupeleka katika eneo la nchi kavu iliyofunikwa na maua makubwa makubwa ya aina tofauti na mimea mengine.

Kisha, utafikia msitu wa milima ya juu unaotoa nafasi kwenye eneo la ajabu la barafu na theluji kama Aktiki.

Kila mbeba mizigo anaweza kubeba kilo 20 tu za mzigo wako ikiwa una zaidi utahitaji kuajiri zaidi ya mmoja. Picha: Tanzania Porters Organisation

Na hapa utakuwa umetimiza lengo lako la kuupanda mlima Kilimanjaro.

Serikali ya Tanzania inasema kila mwaka kati ya watu 30,000 na 50,000 kutoka maeneo mbalimbali duniani hufika kuupanda mlima huu.

Kwa wakati mmoja, unaweza kupata angalau watu 1500 mlimani.

Kwa hivyo, badala ya kuuangalia Mlima Kilimanjaro kutoka Kenya, vuka tu mpaka hadi nchini Tanzania uanze safari ya kuupanda Mlima huo mrefu, ambao ni fahari ya Afrika.

TRT Afrika