Mkutano wa COP 28 unafanyika Dubai, katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu, UAE /Picha TRT Afrika

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia nchi, COP28 umeanza jijini Dubai iliyo katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu, UAE.

Mkutano huo utafanyika kuanzia Novemba, 30 hadi Desemba 12, 2023.

Viongozi wa dunia na wadau mbalimbali wanakutana kwa mwito mkubwa wa kuharakisha hatua za pamoja za kupambana na athari za mabadiiko ya tabia nchi.

Mkutano huo unafanyika katika kile ambacho tayari kinajulikana kuwa mwaka wa joto zaidi kuwahi kutokea katika historia.

"Zaidi ya viongozi 160 wa dunia wanaelekea Dubai, kwa sababu ni ushirikiano kati ya mataifa pekee ndio unaweza kurudisha ubinadamu katika mbio hizi. Lakini COP28 haiwezi kuwa nafasi ya mapicha tu. Viongozi lazima watoe ujumbe - ujumbe uko wazi," Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia nchi Simon Stiell amesema.

"Na wakati viongozi wanaondoka Dubai baada ya mkutano wa kilele, ujumbe wao lazima uwe wazi na sawa: usirudi nyumbani bila makubaliano ambayo yataleta mabadiliko ya kweli."

Unafanyika pia wakati kuna athari tofauti wa mabadiliko ya tabia nchi zikisababisha uharibifu usio na kifani kwa maisha ya binadamu na riziki kote ulimwenguni.

Wanaharakati wa masuala ya hali ya hewa wanasema nchi zilizondelea lazima ziwajibike katika kukumbana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi duniani/ Picha: TRT Afrika

Jinsi ya kutimiza ahadi za ufadhili wa njia za kukumbana na mabadiliko ya tabia nchi ndio msingi wa mkutano huu.

Viongozi wanatarajiwa kujadili jinsi ya kujaza tena hazina ya mabadiliko ya hali ya hewa, kuongeza maradufu rasilimali za kifedha kwa ajili ya uendeshaji wa "hazina ya hasara na uharibifu" yaani 'loss and damage fund', uamuzi muhimu ambao ulitolewa na marais katika mkutano wao wa COP27 mwaka uliopita.

Mkutano wa COP27 nchini Misri uliangazia mageuzi ya kimataifa kwa uchumi wa chini wa kaboni unatarajiwa kuhitaji uwekezaji wa angalau dola trilioni 4-6 kwa mwaka.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anahudhuria mkutano wa COP 28 , Dubai / Picha ya  Abiy Ahmed

"Nchi zilizoendelea zilifanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba michango katika Mfuko wa hasara na uharibifu inabaki kuwa ya hiari, " anasema Rachel Cleetus, mkurugenzi wa sera katika muungano wa wanasayansi.

"Acha niwaambie, kwamba hakuna chochote cha hiari kuhusu athari mbaya na kupoteza maisha ambayo watu wanapata kutokana na mabadiliko ya tabia nchi" anasema Cleetus.

Afrika ina mzigo mkubwa

Athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaonekana katika maeneo tofauti ya bara la Afrika.

Afrika inachangia kwa uchache zaidi katika mabadiliko ya hali ya hewa ilhali ndio inayoathiriwa zaidi na athari zake.

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amefika Dubai katika mkutano wa COP28/ Picha. rais Hakainde Hichilema

Wataalamu wanasema nchi za Kiafrika ambazo zinachangia kidogo sana zitalazimika kutumia hadi mara tano zaidi kukabiliana na mzozo wa hali ya hewa kuliko katika huduma za afya.

"Hizi ni ishara kwamba hatufanyi vya kutosha kushughulikia tatizo la hali ya hewa. Mabadiliko haya yanaambatana na kuongezeka kwa njia za makosa ya kijiografia kati ya nchi za Kaskazini na Kusini mwa dunia, haswa juu ya masuala ya ufadhili wa hali ya hewa," amesema Tasneem Esop, mkurugenzi mkuu wa CAN International,

Wataalamu wanazitaka nchi zilizoendela kutofanya maamuzi ambayo yanaegemea upande mmoja.

"Wachafuzi wa mazingira hawawezi kuandika sheria za mazungumzo haya, tutaendelea kushindwa katika utekelezaji, hadi hapo sekta ya mafuta itakapoondolewa katika majadiliano ya COP," Rachel anaongezea.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atahudhuria mkutano wa COP28 / picha Ikulu Tanzania

Marais na viongozi kutoka bara la Afrika pia wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huu na kuwakilisha msimamo wao ambao ulidhihirishwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika wa mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika nchini Kenya Septemba mwaka huu,

"Sekta ya mafuta inahitaji kulipishwa kutokana na uharibifu na madhara ambayo imesababisha. Hakuna kukosekana kwa pesa lakini kutokuwepo kwa hatua ya serikali kufanya sekta ya mafuta na wachafuzi wengine wakubwa walipe," Shirka la kutetea mazingira la Green Peace initiative limesema katika taarifa yake.

"Serikali katika mkutano wa COP28 lazima zionyeshe kuwa ziko makini kuhusu hatua ya mabadiliko yahali ya hewa kwa kuthibitisha kanuni ya ‘mchafuzi alipe’ katika makubaliano yao," imeongezea.

TRT Afrika