Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Serikali ya Tanzania imetangaza kumrudisha kazini aliyekuwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii nchini humo, Dkt Nyambura Moremi.
Dkt Moremi, ambaye pia ni mtaalamu wa Mikrobiolojia, alisimamishwa kazi mwaka 2020 na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kwa wakati huo, John Pombe Magufuli kukataa vipimo vya maabara hiyo kuhusu uwepo wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona.(UVIKO-19) nchini Tanzania.
Hayati Magufuli alihoji uhalali wa vipimo vilifofanywa na maabara hiyo na kukana uwepo wa Uviko-19 nchini Tanzania.
Kulingana na kiongozi huyo, vipimo hivyo vilitoka kwenye mapapai, ndege na mbuzi na kuaminisha umma kuwa vilitoka kwa binadamu.
Hayati Magufuli alihoji uhalali wa vifaa vya maabara hiyo pamoja na wafanyakazi wake, na kukataa wazi matokeo ya maabara hiyo.
Hatua hiyo iliilazimu Wizara ya Afya kuunda tume ya watu 10 kuchunguza mwenendo wa maabara hiyo ya taifa na kwamba itatakiwa kuwasilisha taarifa yao ifikapo tarehe 13 Mei, 2020.
Rais Magufuli atakumbukwa kwa msimamo wake wa awali kuhusu ugonjwa wa Uviko-19 ambao, ulitofautiana na viongozi wengine duniani.
Kwa mfano, kiongozi huyo alikana uwepo wa ugonjwa huo na kusisitiza kuwa sala na maombi yameinusuru nchi hiyo, huku akapiga marufuku kuchapishwa ripoti kuhusu idadi ya mambukizi au vifo vilivyotokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani kufuatia kifo cha ghafla cha Magufuli, Rais Samia Suluhu aliweka wazi kuwa kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo," Wanaokataa kuwa haupo janga hili halijawafika wao au familia zao
Muda mfupi baadae, Tanzania ilitangaza kuzindua Mpango Mkakati wa Upatikanaji Chanjo Duniani wa dola za Marekani milioni 25, utakaowezesha upatikanaji wa chanjo.