Mafuriko hayo yanajiri wakati ambapo zaidi ya watu 800,000 wa kaunti hiyo ya wafugaji wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na wanategemea misaada ya kimataifa./ Picha: AFP

Pembe ya Afrika iliyokuwa ikikabiliwa na ukame mbaya zaidi uliowaacha mamilioni ya watu bila chakula, sasa inakabiliwa na mvua kubwa za El Nino zilizosababisha mafuriko yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mafuriko hayo yameharibu barabara kuu inayoelekea Garissa, majirani wa Kaskazini Wajir na Mandera na kukata barabara kuu ya inayoelekea Nairobi, huku ikikwamisha watumiaji wa barabara hiyo ikiwemo mamia ya magari ya mizigo.

Maafa ya hivi karibuni yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kusababisha idadi kubwa ya watu kuhama makwao nchini Kenya, Somalia na Ethiopia.

Kwa Fatuma Hassan Gumo, siku chache baada ya mafuriko kufunika nyumba yake mashariki mwa Kenya, alilazimika kupita kwenye maji yenye kina kirefu ili kuokoa maisha yake, na baadhi ya vitu vilivyosalia.

Mafuriko hayo ya ghafla kutoka mto Tana mjini Garissa, kaunti inayopakana na Somalia, yamemlazimisha muuzaji huyo wa matunda mwenye umri wa miaka 42 kuondoka yeye na familia yake katika makazi yake yaliyosombwa na mafuriko usiku hadi nchi kavu.

Yeye ni miongoni mwa maelfu ya watu walioachwa bila makazi kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini Kenya, na kuwaua zaidi ya watu 70.

"Maji haya yameharibu kila kitu," Fatuma aliyeonyesha kufadhaika aliiambia AFP, bila kuzingatia hatari za kiafya baada ya kufurika kwa shimbo la choo.

"Maisha yangu yako katika hali mbaya sana hivi sasa."

Mamia ya watu wamelazimika kustahimili mvua zilizonyesha kwa sik nne mfululizo, huku wakilala katika mazingira hatarishi, kabla ya kupata msaada mahema kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, hayo ni kwa mujibu wa mshonaji mikeka mwenye umri wa miaka 60, Amina Duke Gabuku.

Hata hivyo, kuna wasiwasi mkubwa kwamba hali mbaya ya usafi wa kambi na ukosefu wa maji safi inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupindu.

Kambi 18 kama hizo zimeanzishwa mjini Garissa ndani ya muda wa majuma mawili, zikiwa na watu zaidi ya 7,000.

Mafuriko hayo yanajiri wakati ambapo zaidi ya watu 800,000 wa kaunti hiyo ya wafugaji wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na wanategemea misaada ya kimataifa.

AFP