Mfalme wa Morocco alionyesha mshikamano na taifa lake lililokuwa likipitia wakati mgumu huku likiendelea kukadiria maafa kutokana na tetemeko baya la ardhi.
Mfalme Mohammed VI aliwazuru baadhi ya waliojeruhiwa hospitalini karibu na kitovu cha tetemeko hilo ambako pia alichangia damu.
Pia Mfalme Mohammed alikagua hospitali iliyopewa jina lake Katika Jiji la Marrakech, ambapo alifuatilia huduma na utunzaji unaotolewa kwa wale waliojeruhiwa katika tetemeko hilo la Ijumaa usiku, shirika rasmi la habari la MAP lilisema
Video imemuonyesha mfalme - ambaye kwa kawaida huwa ni nadra kuonekana hadharani isipokuwa matukio maalum, akiwa kando ya kitanda cha wagonjwa na kuwapa busu kichwani baadhi ya waathiriwa.
Tetemeko hilo la ardhi, lenye kitovu chake katika Milima Ya Atlas, liliua watu zaidi ya watu 2,900 — wengi wao wakiwa katika miji na vijiji vya milimani na kujeruhi wengine zaidi ya 2,000. Kufikia Jumanne, zaidi ya majeruhi walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali kuu katika mkoa wa Marrakech.
Aidha, tetemeko hilo pia liliharibu sehemu za kuta zinazozunguka jiji la kale La Marrakech, eneo la urithi wa dunia wa UNESCO lililojengwa katika karne ya 12.