Na Kevin Philips Momanyi
Vilio, mayowe na hali ya kukata tamaa ilitawala sehemu kubwa nchini Morocco, hasa katika maeneo yaliyoathariwa na tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo tarehe 11 September mwaka huu.
Wataalamu wa majanga wanasema, hili ni tetemeko kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini huko katika kipindi cha zaidi ya miongo mitano.
Taarifa kutoka mamlaka nchini humo, zinasema, zaidi ya watu 2,900 wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 5,500 kujeruhiwa na kupoteza makazi.
Athari za tetemeko hilo ilisikika katika nchi tatu ambazo ni Algeria, Ureno na Uhispania.
Lakini wengi wamekuwa wakijiuliza, ni nini hasa kilichofanya tetemeko hili la ardhi kuwa na athari kubwa zaidi na hata kusababisha maafa kiasi hicho?
Wataalamu wanasema, madhara ya tetemeko la ardhi yanaweza kuchangiwa na vigezo kadhaa kama vile umbali wa watu kutoka kwenye tetemeko la ardhi, aina ya udongo uliopo katika eneo la tukio, ujenzi wa majengo na muda wa tetemeko.
Uharibifu haufanyiki kwa kawaida hadi ukubwa wa tetemeko la ardhi ufikie mahali fulani yaani kupita kipimo cha 4 au 5 kulingana na wanasayansi wa dunia au kwa kimombo seismologists.
Mawimbi ya tetemeko la ardhi
Tetemeko la Morocco lilikua la kipimo cha juu sana 6.8, japo lilikua la kina kifupi.Kuna aina tatu za matetemeko ya ardhi.
Tetemeko la kina kirefu, kina cha katikati na kina kifupi. La kina kirefu ni lile linalofanyika kati ya kilomita 0 hadi 70 chini ya ardhi, huku la kati hufanyika kati ya kilomita 70 mpaka 300 chini ya ardhi na kina kirefu ni lile linalofanyika kina cha zaidi ya kilomita 300.
Kwa ujumla, matetemeko ya ardhi yenye kina kifupi husababisha uharibifu mkubwa zaidi kuliko yale ya kina kirefu.
Mawimbi ya tetemeko la ardhi kutoka kwa kina kirefu chini ya ardhi lazima yasafiri umbali mkubwa zaidi kabla ya kusikika juu ya ardhi.
Hivyo basi, yanakuwa na madhara madogo kwa sababu tayari huwa yamepoteza makali yake.
Lakini tetemeko la kina kifupi chini ya ardhi linasafiri umbali mdogo zaidi kabla ya kusikika juu ya ardhi.
Tetemeko la Morocco
Tetemeko la Morocco lilikuwa la kina kifupi ndio maana lilisababisha madhara makubwa zaidi.
Hivyo basi, madhara yake yanakuwa makubwa zaidi.
Vilevile, majengo katika eneo lilioathiriwa yalikua ya zamani tofauti na nyumba zilizopo katika miji ya kisasa ya Morocco.
Tetemeko hilo pia lilitokea saa tano ya usiku, ambapo watu wengi walikuwa tayari wamelala hasa watoto ambao walikuwa ndio waathirika wakubwa.
Kulikuwa pia na matetemeko madogo yaliyofuatia tetemeko kuu lenyewe na kuchangia maafa na uharibifu zaidi.
Wakati misaada kibinadamu ikiendelea kuwasili nchini Morocco, bado haijulikani jinsi nchi hiyo itakavyotibu majeraha yake na kujijenga upya.