Waathiriwa wengi hawajapokea msaada huku serikali ya Morocco ikisemekana kukataa msaada wa baadhi ya nchi /Picha : Reuters

Vidole vya lawama vimeanza kunyooshewa serikali ya Morocco kufuatia maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi la Ijumaa usiku.

''Tumesubiri usaidizi muda mrefu,'' Jamal Rbaki, mkaazi wa Marrakech ameambia shirika la Reuters. ''Sielewi kwanini ilichukua serikali muda mrefu kutufikia, pengine wazazi wangu wangekuwa hai bado,'' ana lalama.

Jamal, ambaye aliwapoteza wazazi wake wote wawili, anasema alisubiri siku nne kabla magari na mashine za kuondoa vifusi kuwafikia katika kijiji chao cha Talaat N'Ya'qoub kando ya mji wa Marrakech.

"Huu ni usaliti. Usaliti mtupu," alisema, na kuongeza kuwa watu walikuwa bado wamenaswa chini ya majengo yaliyoporomoka katika baadhi ya maeneo.

Ufaransa yajitetea kwa wananchi

Jamal alipekua kifusi kwa mikono yake, akisaidiwa na kaka yake, mjomba na majirani huku helikopta za kijeshi zikiruka juu.

Upande wa pili, Serikali ya Ufaransa imetoa tangazo kwa wananchi wa Morocco moja kwa moja, ikiwaeleza kuwa imetamaushwa na maafa yaliyotokea nchini humo kutokana na tetemeo la ardhi.

"Tuna uwezo wa kutoa misaada ya moja kwa moja ya kibinadamu," Macron alisema, akiongeza kuwa ni juu ya Mfalme Mohammed VI na serikali - ambayo hadi sasa imepuuza ofa ya Ufaransa - kuandaa msaada wa kimataifa. "Tunasubiri uamuzi wa serikali huru ya Morocco," Macron alisema.

Watu wengi wamelazimika kulala nje kwa siku ya nne huku waokoaji kutoka Uhispania, Uingereza na Qatar wakisaidia timu za utafutaji za Morocco. Italia, Ubelgiji na Ujerumani zimesema bado zinasubiri kuidhinishwa ofa zao kuja kusaidia.

Huu unatazamiwa kuwa mzozo wa kidplomasia uliofunika hitaji la kimisaada, ambapo Morocco inawakataliwa Wafaransa huku Ufaransa nayo ikichukua fursa hiyo kuichafua serikali ya Morocco kwa wananchi wake.

Paris na Rabat zimekuwa na uhusiano mgumu katika miaka ya hivi karibuni - hasa kuhusu eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi, ambalo Morocco inataka Ufaransa itambue kama himaya ya Morocco. Morocco haijawa na balozi mjini Paris tangu Januari.

TRT Afrika na mashirika ya habari