Mbunifu kutoka Kenya azalisha petroli kwa kutumia taka za plastiki

Mbunifu kutoka Kenya azalisha petroli kwa kutumia taka za plastiki

James Muritu ametengeneza njia mbadala na rafiki kwa mazingira kwa kutumia taka za plastiki.
Jamesa Muritu anatengeneza Petroli na Dizeli kwa kuchoma taka za plastiki. Picha: James Muritu

Na Pauline Odhiambo

Mvumbuzi na mjasiriamali kutoka Kenya James Muritu amebuni njia ya kubadilisha taka za plastiki kuwa mafuta.

"Nilikuwa nikitengeneza vitalu vya kabro kutokana na taka za plastiki, na wakati wa majaribio yangu niliona namna plastiki zinavyoshika moto lilinishangaza," anaiambia TRT Afrika.

Ugunduzi huo ulimfanya James aachane na utengenezaji wa vitalu hivyo na kuamua kuanza kuzalisha mafuta kupitia plastiki zilizoyeyushwa.

Alifanikiwa kufanya hivyo kwa kuziyeyusha plastiki kupitia nyuzi joto za juu kabisa.

"Baada ya kupata mafuta hayo, nilijaribu kuyatumia katika vyombo tofauti kama vile majenereta," anaelezea James, mwanzilishi wa kampuni ya Progreen Innovations, iliyojikita katika kuzalisha mafuta kupitia taka za plastiki.

"Nilijaribu kutumia mafuta hayo kwenye mashine ya kukatia majani na ilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa."

Mchakato rafiki kwa mazingira

Ubunifu huu unalenga kutatua tatizo la taka za plastiki duniani.

Takwimu za Mradi wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) zinaonesha kuwa dunia huzalisha takribani tani milioni 400 kila mwaka.

Asilimia chini ya 10 ya taka hizi hurejeshwa, wakati 12 nyengine huchomwa moto. Idadi kubwa ya taka hizi huishia kwenye madampo na kuchukua miaka mingi kuoza.

James na wenzake hukusanya taka za plastiki, kuzichambua kabla hawajaanza mchakato wa kuzichemsha ili kuzalisha mafuta.

Bidhaa za James hutumika zaidi na waendesha pikipiki, maarufu kama boda boda. Picha: James Muritu

Plastiki zilizosagwa huwekwa kwenye tanuri kwa ajili ya kuchakata.

Mchakato huo huchukua kati ya saa 24 hadi 36, kutegemeana na uzito wa plastiki hizo.

"Tunachofanya ni kinyume na uchomaji moto," James anaelezea TRT Afrika.

"Pamoja na uchomaji, kuna moshi mwingi, na harufu ya sumu ya plastiki inayoungua inajaza hewa. Hakuna gesi inayotolewa katika mchakato wetu, na tunaendelea kutafiti hilo ili kuhakikisha kuwa haina kaboni kwa asilimia 100.

Nafuu kuliko petroli

Mafuta ghafi huzalishwa katika hatua ya kwanza ya usindikaji na kusafishwa baada ya hapo kutengeneza petroli na dizeli.

Njia mbadala ya petroli inaweza kutumika katika injini ndogo na za kati za petroli, wakati dizeli inaweza kuendesha jenereta na mashine nzito zaidi.

James hutumia dizeli anayozalisha mwenyewe kwenye gari lake analolitumia katika shughuli zake za kila siku.

Kupitia kampuni yake, James huzalisha hadi lita 1,000 za mafuta kwa wiki.

James ameweka nia ya kuongeza uzalishaji wa mafuta hadi kufukia lita 20,000 kwa wiki. Picha: James Muritu

Dizeli hiyo huuzwa kwa wamiliki wa malori wanaosafirisha mizigo mikubwa. Wakulima huitumia kuwasha matrekta na vifaa vya umwagiliaji.

Mteja mwingine wa James ananunua dizeli kwa kuchimba visima na mashine nyingine nzito zinazotumika katika ujenzi wa barabara.

Petroli nyingi hununuliwa na waendesha pikipiki za kibiashara, maarufu kama bodaboda .

"Uzuri wa bidhaa zetu ni kwamba inaweza kuchanganywa na petroli au dizeli inayopatikana kwenye vituo vya mafuta," anasema James, ambaye anajitahidi kuongeza uwezo wake wa uzalishaji hadi kufikia lita 20,000 kwa wiki.

"Waendesha boda hununua mafuta yangu kwa sababu ni ya bei nafuu kuliko mafuta ya pampu, na kisha kuyachanganya na mafuta mengine. Wanayafurahia sana huku wakisema kuwa hudumu kwa muda mrefu."

Changamoto za Ufadhili

Ilimchukua James mwaka mmoja kupata vibali kutoka shirika la viwango la nchini Kenya, ili aanze kuuza na kusambaza bidhaa zake.

Kwa sasa anajifadhili, hasa akitegemea akiba kutoka kwenye mshahara wake.

"Watu wengi hawaamini njia nyingine yoyote ya kupata petroli au dizeli isipokuwa kutoka kwa vituo vya kawaida vya mafuta," anasema James.

Pamoja na changamoto hizo, bado anapata muda wa kuwashauri wanafunzi wa uhandisi.

"Inatakiwa ujiamini katika ndoto zako na kuunda uvumbuzi wa kushangaza ambao unaweza kujiuza," anaiambia TRT Afrika.

TRT Afrika