Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Chama cha Mawakala wa Utalii nchini Tanzania (TATO) kinaitaka serikali ya nchi hiyo kutoa ufafanuzi juu ya mpango wa kuanzishwa kwa kodi watakayotozwa watalii wanaowasili visiwani Zanzibar, kuanzia mwezi Oktoba 2024.
Chama hicho, kinataka uwazi kuhusu kiasi cha Dola za Kimarekani 44 ambazo wageni watapaswa kutozwa ili kuingia visiwani Zanzibar kufurahia mandhari ya visiwa hivyo vya karafuu.
Katika mahojiano yake na TRT Afrika, Mwenyekiti wa TATO Wilbard Chambulo amesema ni vyema kwa serikali kutoa ufafanuzi wa jambo hilo kwa manufaa ya utalii wa visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
"Tunataka uwazi kwenye suala hili, ni vyema tukaelimishwa ili tuelewe na tuweze kuwaelewesha wengine," anasisitiza Chambulo.
Kulingana na Mwenyekiti huyo wa TATO, tayari mawakala wanaoiuza Tanzania wameanza kulalamikia mpango huo, ambao unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2024.
"Kabla mtu yeyote hajapanda ndege na kusafiri ni lazima akate bima ambayo itatumika iwapo kutatokea tatizo la aina yoyote ile wakati wa safari au kule anakokwenda, hii bima nyingine ya Dola 44 inatoka wapi?" anahoji Chambulo.
Chambulo anasisitiza kuwa ipo haja kwa wadau wa utalii kupewa ufafanuzi wa namna gani hiyo kodi inafanya kazi, kwani kwa sasa haina maana yoyote.
“Dola 44 haiwezi kuua utalii wa Zanzibar, lakini ni kitu kinachotuletea aibu."
Kulingana na Chambulo, tetesi za uhusikaji wa kampuni ya bima ya Axa kutoka Ufaransa katika mchakato huo, kunaibua maswali zaidi kuliko majibu.
Kwa mujibu wa Chambulo, hapo awali, baadhi wa wajumbe wa Axa walijaribu kuwashawishi TATO kuhusu utekelezwaji wa kanuni hiyo kwa upande wa Tanzania bara, bila mafanikio yoyote.
Mwenyekiti huyo wa TATO anaiambia TRT Afrika kuwa hapakuwa na majadiliano yoyote kati ya serikali na wadau wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa la Tanzania, kuelekea utekelezwaji wa kanuni hiyo.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa upande wa Zanzibar, Dkt Saada Mkuya anatarajiwa kukutana na wadau wa utalii wa nchini Tanzania kujadiliana kuhusu suala hilo.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Septemba 13, 2024 jijini Arusha, Tanzania, kulingana na Mwenyekiti huyo wa TATO.
Zanzibar ilishuhudia ongezeko la asilimia 16.4 ya wageni waliotembelea visiwa hivyo kwa mwaka 2023, ambapo jumla ya watalii 638, 498 walitembelea fukwe na mandhari mbalimbali za eneo hilo.