Washington imemuwekea Dagalo kikwazo cha kusafiri nchini Marekani pamoja na kuzuia mali zake zote zilizo nchini Marekani./Picha:Reuters

Siku ya Jumanne, Marekani ilitangaza kumwekea vikwazo kiongozi wa wanamgambo wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo na wenzake kwa kuhusika na mauaji ya kimbari ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Sudan.

Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amedai kuwa RSF na vikundi washirika vimeendelea kutekeleza uhalifu dhidi ya raia wasio na hatia.

“Marekani imedhamiria kuwawajibisha wale wote waliohuiska na mauaji hayo,” alisema Blinken.

Washington imemuwekea Dagalo kikwazo cha kusafiri nchini Marekani pamoja na kuzuia mali zake zote zilizo nchini Marekani.

“Kwa kipindi cha miaka miwili, amejihusisha na vita kati ya RSF na majeshi ya nchi hiyo, ambapo pia amehusika na mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni wengine bila ya makazi,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na serikali ya nchi hiyo.

Mapigano kati ya RSF na majeshi ya Sudan yalianza Aprili 2023, kabla ya mchakato wa kuunda serikali ya kiraia.

TRT Afrika