Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Maandalizi ya mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika wa marais na viongozi wa nchi yameanza huko Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kawaida wawakilishi wa nchi za Afrika katika Umoja wa Afrika yaani mabalozi huanza kwanza kwa mkutano wao wa kuangalia ripoti ya masuali mbalimbali, na baadae hufuatia mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika ndio wameanza sasa kupanga ajenda itakayojadiliwa na marais pindi watakapokutana kati ya tarehe 17 na 18 mwaka huu.
Mwaka wa 2024, Umoja wa Afrika unalenga zaidi kuhimiza nchi wanachama kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu.
Umoja wa Afrika ni nini?
Mnamo Mei 1963, viongozi wa nchi 32 Huru za Kiafrika walikutana Addis Ababa Ethiopia kutia saini Mkataba wa kuunda taasisi ya kwanza ya bara la Afrika baada ya uhuru, iliyoitwa Shirikisho la Umoja wa Afrika (OAU).
Malengo ya OAU yalikuwa ni kulitoa bara katika mabaki ya ukoloni na ubaguzi wa rangi; kukuza umoja na mshikamano miongoni mwa Mataifa ya Afrika, kuratibu na kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya maendeleo.
Nchi za Afrika zikaamua Julai 2002 kuunda Umoja wa Afrika, AU kuendeleza tu kazi yake.
Ili kujiunga na AU, inafaa nchi kuandika barua kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambaye ataipitisha barua hiyo kwa marais kujadiliwa.
Baadae uamuzi unapitishwa iwapo utaungwa mkono na nchi nyingi zaidi. Kwa sasa nchi zote za Afrika ni wananchama. Nchi zote za Afrika ni wanachama wa AU.
Na iwapo nchi yoyote itataka kujitoa kutoka umoja wa Afrika, basi itatakiwa kuandika barua nyengine kwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ambaye ataiwasilisha kwa marais kwa ajili ya kujadiliwa.
Baada ya mwaka mmoja, iwapo nchi inayotaka kujitoa itakuwa haijabadilisha nia yake, basi hapo itakuwa huru kujitoa.
Kwa mfano, Morocco iliwahi kujitoa kutoka Muungano huo mwaka 1984, na hatimae ikajiunga tena kama mwanachama mwaka 2017.
Serikali ambazo zitaingia madarakani kwa njia zisizo za kikatiba yaani kupitia mapinduzi zinasimamishwa kushiriki katika shughuli za Muungano.
Kwa sasa nchi sita zimesimamishwa unachama, baada ya serikali zake kupinduliwa. Nchi hizo ni Mali, Guinea, Burkina Faso, Sudan, Niger na Gabon
Lakini kwa nini Marais na viongozi wa hukutana kila mwaka ?
Kuna mikutano miwili ya kawaida ya viongozi wa Afrika. Imekuwa desturi kwamba Mwanzo wa mwaka wanakutana katika makao makuu ya tume ya Umoja wa Afrika iliyo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mkutano wa pili hufanyika katika nchi nyengine ambayo inaweza kujitolewa kuwa mwenyeji wa mkutano. Viongozi hukutana hasa kujadili masuala nyeti yanayoathiri nchi za Afrika.
Na kila mwaka masuala ya amani na usalama yamekuwa ajenda kuu. Marais wanaweza kutoa uamuzi kwa ajili ya kusuluhisha tatizo katika nchi, lakini lazima nchi husika ikubaliane na uamuzi huo wa kibara kwa sababu kila nchi iko huru.
Uendeshaji wa Umoja huu wa kibara una changamoto yake, mfano ingawa kila nchi inafaa kutoa kiasi cha fedha kuchangia katika shughuli za kibara, bado ufadhili zaidi ya asili mia 50 ya miradi tofauti za Umoja wa Afrika inatoka kwa nchi za kigeni.
Pia kuna changamoto ya nchi kutotii maamuzi ya Umoja wa Afrika.
Licha ya changamoto hizi nchi zetu za Afrika zimefanya mipango mingi ya kimaendelea, ikiwemo mpango wa Afrika wa kujenga biashara zaidi katika ya nchi za Afrika, kujitahidi kuleta usalama katika nchi zenye changanmoto hii na kuboresha afya.
Hata hivyo, wakati marais wakipanga kukutana tena, changamoto ya amani na usalama katika baadhi ya maeneo bado inaonekana kuwa tatizo.
Na mara nyingi, Umoja wa Afrika umekuwa ukinyooshewa kidole kwamba, kwa kiasi fulani, umeshindwa kukidhi matarajio ya wengi, hasa panapoibuka migogoro mikubwa ya kikanda.