Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa uchambuzi wake juu ya mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, ikionya kuzuka kwa ugonjwa wenye kuathiri mfumo wa mapafu, unaojulikana kitaalamu kama Nimonia.
"Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo," imesema TMA katika taarifa yake.
Vilevile, mamlaka hiyo imeonya uwezekano wa uwepo wa magonjwa ya macho utakaosababishwa na vumbi linalotokana na upepo katika baadhi ya maeneo Tanzania.
TMA pia iligusia mwelekeo wa hali ya upepo ikisema kuwa msimu wa kipupwe wa 2024 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki katika maeneo mengi ya Tanzania na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.
Mamlaka hiyo pia ilitoa mwelekeo wa mvua ikitabiri vipindi vya mvua vitakavyotarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.