Idadi kubwa ya wafungwa wametoroka kutoka gereza lenye ulinzi duni nchini Comoro, mamlaka ya nchi hiyo imesema.
Maafisa kutoka visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi walisema wafungwa 38 walitoroka jela hiyo yenye watu wengi katika mji mkuu Moroni, baada ya kusaidiwa na mwanajeshi aliyekuwa kizuizini.
"Hata sikupata muda wa kuswali swala ya Eid al-Fitr. Tukio hilo limetokea mapema sana," Soilihi Ali Said, mkuu wa huduma ya magereza, aliiambia AFP.
Waendesha mashtaka wa nchi hiyo wanasema kuwa wafungwa hao walitumia mwanya wa uzembe kwenye ulinzi wa gereza hilo kufanikisha azma yao.
Uzembe kwenye ulinzi
"Chanzo kikuu cha kutokea kwa tukio hili ni uzembe kwa upande wa walinzi," amesema mwendesha mashtaka wa nchi hiyo Ali Mohamed Djounaid.
"Wafungwa hao walitumia mwanya huo na kutorekea kupitia lango kuu la gereza hilo."
Kulingana na Djounaid, inasemekana kuwa, mwanajeshi anayeshikiliwa kufuatia kifo cha shabiki wa soka ambaye alipigwa risasi na vikosi vya usalama wakiwazuia wafuasi wake kabla ya mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka jana, ndiye aliyeratibu zoezi hilo la kutoroka kwa wafungwa hao.
"Kitendo hicho kiliratibiwa na askari aliyefyatua risasi kwenye uwanja wa mpira wa Malouzini huko Moroni na kusababisha kifo cha kijana Fahad Moindze," alisema.
Djounaid amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Mwanajeshi huyo ni mmoja ya watu waliotoroka, na hakuna hata mmoja aliyekamatwa hadi sasa, alisema kiongozi huyo wa magereza.
Vitendo vya kutoroka jela vimekuwa ni vya kawaida katika nchi hiyo yenye watu 870,000.
Ikiwa na uwezo wa kuchukua nafasi 90, gereza la Moroni lilikuwa na wafungwa zaidi ya 200, kulingana na Ali Said. Hapo awali, ilidaiwa kuwa gereza hilo limekuwa katika mazingira mabaya sana kwa wafungwa.