Takriban watu tisa waliuawa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa katika ajali ya jengo lililoporomoka katika kitovu cha kibiashara cha Douala nchini Cameroon.
Jengo hilo la ghorofa nne liliangukia jingine dogo mapema Jumapili asubuhi, mamlaka ilisema.
"Takwimu za majeruhi zinaweza kuwa kubwa zaidi. Wafanyakazi wa uokoaji, wakisaidiwa na wanajeshi wa serikali ya Cameroon, bado wanachimba mabaki kuona kama miili zaidi inaweza kupatikana," alisema Samuel Dieudonne Ivaha Diboua, gavana wa eneo la Littoral la Cameroon.
Kikosi cha zima moto cha jeshi kimeamriwa kuungana na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo na huduma nyingine za uokoaji katika kutafuta manusura walionasa chini ya vifusi.
Mshtuko mkubwa kwa wakazi
Wakaazi wanaoishi katika mtaa wa Ndogbon ambapo kisa hicho kilitokea walisema wamepatwa na mshtuko.
"Tulisikia watu wakipiga kelele ... na tulijitahidi kusaidia baadhi ya watu kutoka kwenye mabaki, lakini hatukuweza kufanya hivyo kwa kutumia majembe yetu," alisema Gaspard Ndoppo, ambaye anaishi karibu na majengo yaliyoporomoka.
Kuporomoka kwa majengo hutokea mara kwa mara huko Douala, wakati mwingine kutokana na majanga ya asili kama vile maporomoko ya ardhi na nyakati nyingine kwa sababu ya ujenzi duni, wenyeji wanasema.
Baraza la jiji la Douala kwa sasa linabomoa nyumba katika maeneo hatarishi yanayoathiriwa na mafuriko au maporomoko ya ardhi.
Jengo lililoporomoka siku ya Jumapili halikuwa limelengwa kwa ubomozi.