Kitongoji cha Mathare, kilichoko Mashariki mwa jiji la Nairobi, ni nyumbani kwa watu laki kadhaa japo makazi yenyewe ni duni na sio rasmi,/ Picha: reuters 

Waokoaji wamewatoa watu wanne kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka katika kitongoji cha Mathare katika mji mkuu wa Kenya siku ya Jumanne, lakini kuna uwezekano watu zaidi wamenaswa, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema.

"Watatu kati ya wanne waliookolewa wamepelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu, huku mmoja aliyekuwa na majeraha madogo akipatiwa matibabu katika eneo la tukio," Shirika la Msalaba Mwekundu liliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Jengo la orofa tano lililoporomoka lilikuwa linabomolewa kwa sehemu na maafisa wiki moja iliyopita, lakini baadhi ya wakazi walibaki katika vyumba vyao, alisema Wanjiru Wanjiru, mwanaharakati wa Mathare Social Justice Centre, kikundi cha kutetea haki za mitaa.

"Bado tunatatizika kutokana na mzozo huu wa kiikolojia. Nadhani watu hawakuwa wakiondoka kwa sababu serikali ilikuwa haijawapa watu pesa za kuishi mahali popote," Wanjiru aliambia Reuters kwa njia ya simu.

Kitongoji cha Mathare, kilichoko Mashariki mwa jiji la Nairobi, ni nyumbani kwa watu laki kadhaa japo makazi yenyewe ni duni na sio rasmi, na inalaumiwa kwa kutotii kanuni za ujenzi.

Mathare ilifurika mwezi huu wakati mto unoapita kati yake, ulipasua kingo zake baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha vifo vya watu kadhaa na kuwalazimisha maelfu ya watu kuondoka makwao.

Baada ya majuma kadhaa ya mvua kubwa iliyosababisha vifo vya takriban watu 289 kote nchini, Rais William Ruto mwezi uliopita aliamuru wakaazi kuondoka katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko likiwemo eneo la Mathare, ambako mamlaka ilianza kuharibu makazi kwenye ardhi iliyochukuliwa kuwa haramu.

TRT Afrika na mashirika ya habari