Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi wa Afrika uliofanyika Nairobi, Septemba 4 hadi 6 mwaka 2023. / Picha: AFP

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mtoto anaruka mtaro wa maji machafu huku mama yake akimfokea na kumwambia awe muangalifu.

Sauti yake inapambana na kelele kubwa iliyosababishwa na mwanamume kwenye kipaza sauti akiwaita watu wajiunge na kampeni ya jumuiya.

“Twendeni, twendeni,” anapaza sauti.

Mose Wanja, mratibu wa Jumuiya ya Mathare Social Justice, Shirika la kijamii, anaongoza vijana wengine kwenye Mto ambao umekuwa sehemu ya Jumuia hii lakini umejaa uchafu. Huu ni Mto Nairobi.

Mto Nairobi unaopita katikati ya makazi duni ya Mathare ni chanzo cha maji kwa wakaazi wa jiji katika eneo hili.

Wakulima wadogo wadogo, katika kijiji hiki chenye msongamano wa watu zaidi ya lakini mbili wanatumia maji kutoka mto huu kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga.

Wanja na wenzake wanafanya kampeni kwa jina Ecological Justice, ambayo lengo lake kuu ni kufanya maeneo ya makazi duni kuwa rafiki kwa mazingira.

"Tulifikiria kuwa katika haya yetu ya Mathare hatuna miti karibu," Wanja anaelezea TRT Afrika, "Hivyo tukafikiria wazo la kuipa Mathare kijani kibichi na kuipamba."

Vijana wakazi wa  Mathare walianza mradi wa kusafisha Mto Nairobi na maeneo ya karibu mwaka wa 2014 /Picha: TRT Afrika 

Vijana hawa wa Mathare walianza mradi huu mwaka wa 2014, wakisafisha eneo lililo karibu na Mto kwa kuondoa uchafu uliokuwa umejaa hapo, ili kupanda miti na kutengeneza nafasi ya watoto kucheza.

"Miti ni maalum sana, ni tiba kuwa sehemu yenye miti," Wanja anasema. “Hili lilikuwa jalala au dampo. Tulilidai tena kutoka kwa jamii na tukaliita Hifadhi ya Jamii ya Mathare. Ilikuwa ni dampo lakini sasa unaweza kuona ni sehemu salama kwa vijana,” Wanja anaongeza.

Hifadhi ya eneo kando ya mto bado unaendelea pole pole kwa sababu kikundi hiki kinategema watu kujitolea kuwasaidia.

Takataka zinaedelea kuondolewa na sehemu ya watoto zilizotengenezwa kwa njia za kienyeji zimewekwa. Wazazi wanaendelea kuleta watoto wao hapa huku watoto wengine wanakuja wenyewe.

Vijana wa Mathare wamechukua masuala ya mazingira mikononi mwao, kwa nia ya kuchangia vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, kwani wanasema msaada kutoka kwa serikali huenda ukachelewa kuja kwa wakati unaohitajika.

Nje ya mpaka nchini Uganda mwanamume ambaye amepewa jina la utani na watoto kama "jenerali wa miti" anajiandaa na tamasha lake la kila mwaka la kijani.

Joseph Masembe, mwanaharakati wa mazingira huwaandalia watoto tamasha kila mwaka ambapo hufundishwa umuhimu wa kupanda miti.

Mradi wake "Little Hands Go Green," umekuwa maarufu miongoni mwa watoto ambao lengo kuu ni kupata miche ya miti bila malipo mwishoni mwa ngoma na kucheza.

"Mwaka 2012 nilianza mradi huu rahisi, nikiwa na dhana na imani kwamba ninaweza kumshawishi kila mtoto nchini Uganda kupanda na kumiliki angalau mti mmoja wa matunda," Masembe anaiambia TRT Afrika.

Joseph Masembe kupitia mradi wake " Little Hands Go Green" hutembelea mashule kuhimiza watoto kupanda miti. Picha/Joseph Masembe.

"Kuzingatia kuwapa watoto miche ya matunda ni muhimu kwa sababu ya thamani ya lishe. Katika tamaduni zetu za kale za Kiafrika ni nadra sana kupata mtu akikata mti wa matunda na tunataka kurudisha hilo kwa kuwatia moyo watoto kupenda miti aina hiyo,” Masembe ameongezea.

Miaka 11 baadaye, Masembe amepeleka kampeni yake katika shule za msingi ambako anapeleka miche ya matunda bure kwa watoto kote nchini.

"Wazo la kuhifadhi mazingira linategemea watoto ambao watakuwa na maisha ya baadaye kwa muda mrefu baada ya wengi wetu kuondoka," anasema.

Azimio la Nairobi na kupunguza Kaboni

Wanja na Masembe ni baadhi ya Waafrika ambao wanatarajia mengi kutoka kwa maazimio ya viongozi wa Afrika baada ya mkutano wao wa mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2023.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza wa aina yake barani huku kukiwa na tamko kali kutoka kwamba dunia haiko salama kutokana na ongezeko la joto duniani hadi 1.5C, kama nchi zilizokubaliana jijini Paris mwaka 2015, na kwamba uzalishaji wa gesi chafu duniani lazima upunguzwe kwa asilimia 43 mwaka huu.

Baadhi ya wananchi kutoka mataifa mbalimbali waliandamana jijini Nairobi Septemba 2023, wakati wa Mkutano wa Afrika wa Mabadiliko ya tabia nchi/ Picha: AFP 

Viongozi wa Afrika walibainisha kuwa licha ya Afrika kuwa na makadirio ya asilimia 40 ya rasilimali za nishati mbadala duniani, ni dola bilioni 60 tu au asilimia mbili ya uwekezaji wa nishati wa dola za Kimarekani trilioni 3 katika muongo uliopita, uliofika Afrika.

"Tunatoa wito kwa viongozi wa dunia kutambua kwamba kuondoa kaboni katika uchumi wa dunia ni fursa ya kuchangia usawa na ustawi wa pamoja," tamko la Nairobi lilisema.

Utoaji kaboni unamaanisha kubadili kutoka kwa matumizi ya nishati ya visukuku kama vile makaa ya mawe, gesi asilia au mafuta hadi vyanzo vya nishati visivyo na kaboni na nishati mbadala.

Kulingana na Azimio la Nairobi, mageuzi ya kimataifa kuwekeza zaidi katika kaboni yanatarajiwa kuhitaji uwekezaji wa angalau dola trilioni nne hadi sita kwa mwaka, na kutoa ufadhili kama huo kunahitaji mabadiliko ya mfumo wa kifedha na miundo na michakato yake, kushirikisha serikali, benki ya Dunia, benki za biashara, wawekezaji wa taasisi na wahusika wengine wa kifedha.

"Pato la Taifa linahusu mikopo, ni kuhusu mali. Tuna mifereji ya kaboni inayohudumia ulimwengu, ambayo husafisha mazingira yetu, hufanya kama unyakuzi wa kaboni ambayo inatolewa na wengine lakini hatupati chochote katika hilo," rais wa Kenya William Ruto aliambia mkutano huo.

"Ili kufungua rasilimali ambazo tunahitaji kuendesha, uwekezaji huu mpya na fursa za kifedha, hasa katika nishati ya kijani, tunaamini ni wakati wa kuwa na mazungumzo kuhusu kodi ya kaboni," aliongeza.

Wataalamu wanasema misitu ya Afrika inachukua tani milioni 600 za CO2 kila mwaka, zaidi ya mfumo wa ikolojia wa misitu duniani.

Kufunguliwa kwa masoko ya mikopo kumeanza kuvutia maslahi mengi ya kimataifa barani Afrika, na hivyo kuzua wasiwasi wa uwezekano wa nchi kutoa ardhi kwa wazabuni wa juu na bado nchi nyingi za Afrika hazina sheria zinazofaa.

Kenya, ambayo ilitoa wito huo, ilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Tabia nchi 2023 iliyorekebishwa mnamo Septemba kuiruhusu kuunda usajili wa kitaifa wa kaboni na kuteua mamlaka ya kuiendesha.

"Hatujatoa hata inchi moja ya ardhi kwa mtu yeyote kwa kweli tunakamilisha kanuni zao," rais Ruto aliwaambia wanahabari katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi COP28 huko Dubai.

"Tunafanyia kazi kanuni kwa sababu tunataka kuleta uadilifu katika eneo zima la kaboni, bei ya kaboni, masoko ya kaboni, biashara ya kaboni. Tunataka kuhakikisha kuna uadilifu wa kutosha,” aliongeza.

Benki ya Dunia inaripotiwa kufanya hima kusaidia nchi za Afrika kuweka kanuni zinazofaa kwa soko la kaboni.

Mapato ya kaboni yatawafikia wananchi?

Huko Nairobi, Kenya kundi jengine la vijana wanaohusika na usafishaji wa aMto Nairobi wamekuwa wakifuatilia Azimio la Nairobi.

Humprey Omukuti anaongoza juhudi za hiari zinazolenga kurejesha sehemu nyingine ya Mto Nairobi ambapo Wanja na vijana wengine ambao pia wanajitahidi kuwa na kijani kibichi katika eneo la makazi mapya la Mathare.

Kundi lao linaitwa "Ghetto Farmers," na wanaamini kwamba kupanda mianzi kando ya mto uliochafuliwa kunaweza kuokoa.

"Nimefuatilia kwa karibu tamko la viongozi wetu mwezi Septemba na nilipendezwa sana walipoangazia mikopo ya kaboni kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa," Omukuti anaiambia TRT Afrika.

Anasema hakuna utata kuhusu hilo kwa sababu linahusu upandaji miti.

"Swali letu ni je, pesa ambazo serikali zetu za Kiafrika hupata kutokana na mikopo ya kaboni zitaingia kwenye makundi yaliyopangwa kama yetu ambayo tayari yanapanda miti kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe?" anauliza.

“Katika miji yote hii barani Afrika kuna vijana wengi ambao hawana hata ajira, kwa nini tusipate hizo fedha za kaboni kama taifa, tulipe vijana hawa na wapande miti zaidi? Itakuwa ushindi kwa sababu vijana wataajiriwa na nchi itaboresha eneo lake la kijani kibichi." Omukuti anaongeza.

Changamoto tuliyonayo ni viongozi wetu kutarajia tufanye kazi ya mazingira kwa hiari na wao wanapeleka fedha kwenye makampuni makubwa badala ya kutuunga mkono kupambana na janga hili.

Hili ni bara letu na tungependa kuwa sehemu ya juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa lakini kwa njia ya heshima,” anaongeza.

Omukuti anasema tamko la Nairobi lazima lionekane kufanya kazi barani Afrika na hiyo ina maana kwamba viongozi wa Afrika kushinikiza mataifa yaliyoendelea kumiliki uzalishaji wao wa gesi na kisha kuwekeza kwa hali inayofaa katika mazingira ya kijani kibichi.

TRT Afrika