Na Dayo Yussuf
Ali Khalid amepoteza hesabu ya maiti alizozika - watu wasiowafahamu ambao hawezi kukumbuka majina na sura zao, lakini ambao hisia zake zinabaki zimefungamana nao.
"Katika Uislamu, mtu anapokufa, ni jukumu la jamii kuhakikisha mtu huyo anazikwa ipasavyo," mkazi wa Nairobi anaiambia TRT Afrika.
"Inasikitisha kufikiria kunaweza kuwa na Mwislamu mwenzangu amelala katika chumba cha kuhifadhia maiti karibu nami kwa siku au miezi kadhaa, bila mtu wa kumsitiri maiti yake."
Lakin iAli ni miongoni mwa wachache walio tofauti katika mazingira nyeti ya kitamaduni ambapo hata kuzungumza juu ya kifo kunaweza kuwatia watu kiwewe.
Anaendesha shughuli zake kupitia msikiti mkuu wa Jamia jijini Nairobi, akishirikiana na kikundi kidogo cha watu, ambao wanajitolea kutafuta habari kuhusu miili ya Waislamu ambayo haijachukuliwa na imelazwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti vya umma katika miji mbalimbali Kenya.
Tangu kuanza misheni yake, Ali amewazika watu wengi ambao vinginevyo wangenyimwa sitara ya utu katika kifo.
Makaburi yanajaa
Mnamo Septemba, Kaunti ya Jiji la Nairobi ilitoa notisi kwa umma ikiwataka watu kufika na kuwatambua wapendwa wao ikiwa wametoweka.
Ilisema miili 200 ambayo haijadaiwa ilikuwa imerundikana katika vyumba vya kuhifadhia maiti vya umma katika muda wa mwezi mmoja tu, na kuacha mamlaka bila chaguo ila kuzitupa baada ya muda fulani.
Hospitali ya Kenyatta, kituo kikubwa zaidi cha afya ya rufaa cha serikali nchini, ilikuwa imetoa notisi kama hii mwezi uliopita, ikitoa muda wa siku saba kabla ya kutupa miili 233 iliyokuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa zaidi ya miezi mitatu.
“Tuna mawasiliano katika hospitali mbalimbali na hata vyumba vya kuhifadhia maiti, wakikutana na Mwislamu amefariki na hakuna ndugu aliyejitokeza kuudai mwili huo, wanatufikia basi tunaingilia kati,” anasema Ali.
"Tunajaribu kuwatambua ndugu wa mtu huyo kama tunaweza. Ikiwa sivyo, tunashughulikia mazishi kupitia Waqfu wa Msikiti wa Jamia."
Wanaosaidika wachache mno
Ingawa inafariji kusikia kuhusu utumishi wa Ali na wenzake, wanahudumia asilimia ndogo ya watu.
Kenya ni chini ya chini ya asilimia 20 ya Waislamu, na Ali anasema hutoa huduma za mazishi kwa wale wanaofuata imani yake pekee.
Kwa vile hajui utaratibu wa maziko ya wasio Waislamu ni upi, hofu ya athari za kisheria inamzuia kujitosa zaidi ya kile anachoridhika nacho.
Steven, Mkatoliki mwaminifu, anaiambia TRT Afrika kwamba hali ni ngumu zaidi kwa Wakristo.
“Unaona Wakristo wamegawanyika katika madhehebu mbalimbali, kila moja likiwa na mila na taratibu zake, hasa kuhusiana na mazishi,” anasema.
"Pia, makanisa mengi yana uanachama na usajili, ambayo huja kwa manufaa wakati wa kutoa huduma kama vile ndoa, ubatizo, au taratibu za mazishi. Kwa hiyo, kanisa linawezaje kuchukua mwili wa mtu asiyejulikana na kuuzika?" anauliza Stephen.
Tatizo la mara kwa mara
Kwa miaka mingi, miili ambayo haijakuja kuchukuliwa na kurundikana katika hifadhi za maiti za umma imekuwa changamoto ya kiutawala.
Mnamo Februari, Kaunti ya Jiji la Nairobi ilipata agizo la mahakama la kutupa miili 250 ambayo haikuchukuliwa na wenyewe. Hospitali kadhaa kote nchini zilitoa notisi ya wiki moja kabla ya kutupa miili hiyo katika vyumba vyao vya kuhifadhia maiti.
"Wakati mwingine, tunatafuta familia, lakini tunakuta kwamba hawana uwezo wa kulipa bili za hospitali na kumudu mazishi. Kisha tunakusanya pesa wakati mwingine, kupitia mitandao ya kijamii au misikitini," anasema Ali.
Maiti nyingi ambazo hazijatambuliwa ambazo zimelala bila kuchukuliwa na wenyewe katika vyumba vya kuhifadhia maiti ni za wahasiriwa waliokufa kwa ajali au watu waliokufa ghafla.
Kulingana na Baraza la Kaunti ya Nairobi, kujiua, kupigwa na umeme, kuzama majini, kupigwa risasi na kuuawa ni miongoni mwa visababishi vya vifo vya watu tunaowakuta bila wenyewe mara kwa mara.
"Mtindo wa maisha umebadilika, na watu wengine wanaishi mijini bila mawasiliano na familia zao. Kwa hivyo, jambo linapotokea kwao, hakuna mtu anayejua," anasema Ali.
Anaamini kuwa serikali inaweza kubuni mpango bora wa kuondoa miili hii ambayo haijadaiwa.
"Sheria ya Afya inaweka bayana makaburi ya halaiki kwa ajili ya kutupwa miili ambayo inakuwa haina mazingatio ya kuwapa hadi. Unakuta miili ya kiume na ya kike ikiwa imeunganishwa kama magogo yaliyotupwa kwenye shimo kubwa bila ya kujali," anasema Ali. "Hii sio njia ya kibinadamu ya kumpa mtu sitara."
Ikiwa mahakama mbalimbali zitaidhinisha maombi yanayosubiriwa ya kuondolewa kwa miili, hii itaongeza hadi 500 jumla ya idadi ya mazishi kama hayo mwaka wa 2023 pekee.