Makampuni ya kimataifa yanapanua shughuli za uchimbaji madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hali ambayo imesababisha jamii ya maeneo ya uchimbaji kulazimishwa kuhama makazi na mashamba yao.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty Intrenational pamoja na shirika jengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linaloitwa Initiative pour la Bonne Gouvernance et les Droits Humains.
"Utimuaji huo wa lazima unaofanyika wakati makampuni yanataka kupanua miradi ya madini ya shaba na cobalt ya viwanda yanaharibu maisha ya watu DRC, na lazima yasitishwe sasa," Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International alisema.
Rasilimali za thamani
Kuongezeka kwa mahitaji ya kinachojulikana kama teknolojia ya nishati safi kumeongeza mahitaji yanayolingana ya aina fulani ya madini, pamoja na shaba na cobalt ambayo ni muhimu kwa kutengeneza betri nyingi za lithiamu.
Madini hayo hutumika kuwasha vifaa kama magari ya umeme na simu.
DRC ina akiba kubwa zaidi duniani ya cobalt, na hifadhi ya saba kwa ukubwa ya shaba.
Ripoti hiyo imetoa mfano wa jiji la Kolwezi nchini DRC ambapo jumuiya ya watu zilizoanzishwa kwa muda mrefu zimeharibiwa tangu mgodi mkubwa wa shaba na cobalt ulipofunguliwa mwaka wa 2015.
Mradi huu unaendeshwa na Compagnie Minière de Musonoie Global SAS (COMMUS)- kwa ubia kati ya Zijin Mining Group Ltd, kampuni ya Uchina na Générale des Carrières et des Mines SA (Gécamines), kampuni ya uchimbaji madini ya serikali ya DRC.
Kitongoji kilichoathiriwa cha Cité Gécamines ni makazi ya takriban watu 39,000. Nyumba hizo kwa kawaida huwa na vyumba vingi na zinakuwa katika msongamano. Katika eneo hilo pia, kuna shule na hospitali.
Tangu shughuli za uchimbaji madini zianze tena, mamia ya wakazi wameambiwa waondoke, huku baadhi tayari wakilazimishwa kuhama.
Edmond Musans mwenye umri wa miaka 62, ambaye ni miongoni mwa wanaoripotiwa kulazimishwa kubomoa nyumba yake na kuondoka, alinukuliwa na watafiti akisema:
“Hatukuomba kuhamishwa, kampuni na serikali walikuja na kutuambia, ‘Kuna madini hapa.’”
Edmond na wengine waliofukuzwa walisema fidia iliyotolewa na COMMUS haitoshi kuwanunulia nyumba zinazolingana na makaazi yao.
Majibu kutoka serikalini
Wizara ya Madini nchini DRC inasisitiza kuwa serikali inatilia maanani maisha ya wananchi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanapata manufaa kutokana na shughuli za madini,
Wizara hiyo inaendelea kusema kuwa serikali ya Rais Felix Tshisekedi imefanya mabadiliko katika sheria ya uchimbaji madini kwa lengo la kuhakikisha kizazi kipya cha DRC kinafurahia mapato ya madini ambayo makampuni hasa ya kimataifa yanachimba nchini humo.