Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya Douglas Kanja amekosa kufika mahakamani mara mbili sasa / Picha: AFP

Mahakama nchini Kenya imetishia kumhukumu Inspekta Jenerali wa Polisi wa nchi hiyo iwapo hatafika mahakamani kwa tarehe itakayopangwa.

"Iwapo Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja atakosa kufika mahakamani tena kwa mara ya tatu, sitakuwa na budi ila kumshtaki kwa kudharau mahakama na kumhukumu papo hapo," Jaji Bahati Mwamuye alisema katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Waziri wa Mambo ya Ndani Philip Murkomen waliagizwa na mahakama kufika kotini leo kujibu tuhuma za utekaji nyara.

Hata hivyo hawakufika. Hii ni mara ya pili kwa IGP kukosa kutii amri za kufika mbele ya mahakama.

Waziri wa Mambo ya Ndani Murkomen aliwakilishwa na wakili wake Danstan Omari ambaye alifukuzwa mahakamani kwa madai ya kukiuka sheria kwa kutatiza kesi.

Jaji Mkuu pia ametoa onyo hiyo kwa Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jina, DCI.

Haya yanajiri wiki moja baada ya Mahakama Kuu kumwita Kanja kushughulikia visa vya hivi majuzi vya kutekwa nyara kwa watu kadhaa.

Jaji Mwamuye alimtaka Kanja kuwasilisha watu waliopotea mahakamani, akisisitiza kuwa kutofuata sheria hiyo kunaweza kusababisha adhabu.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imesema katika taarifa kuwa jumla ya kesi 82 za utekaji zimeripotiwa kuanzia Juni 2024.

Vijana sita walioripotiwa kutekwa Disemba 2024 walijitokeza wakiwa hai wakidai kuwa walikuwa wameachwa sehemu tofauti nchini wakajipeleka nyumbani.

TRT Afrika