Mahakama kuu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, imesitisha utekelezwaji wa ushuru mpya uliopangwa kuanza kuanzia, Julai 1.
Seneta wa Kenya, Busia Magharibi, Okiya Omtatah, alikuwa ameenda mahakamani kupinga Mswada wa Fedha wa 2023, ambao uliwasilisha ushuru mpya au wa juu zaidi.
Omtatah alitetea kuwa kuanzishwa kwa ushuru huo mpya ni ukiukaji wa katiba, na kwamba haikuzingatia kandarasi za kibinafsi ambazo Wakenya walitia saini na waajiri wao.
Mnamo Jumatatu, Rais William Ruto aliidhinisha Mswada wa Fedha wa 2023 kuwa sheria baada ya kupitishwa na bunge la taifa la Kenya.
Kodi ya mapato ya juu
Sheria ilileta mezani, ushuru wa nyumba ambao ungetaka wafanyakazi katika sekta rasmi kutoa 1.5% ya mishahara yao kwa mpango wa kitaifa wa nyumba.
Pia ilipandisha ushuru wa mapato kwa watu wanaolipwa mishahara kati ya $3,580 na $5,725 kwa mwezi - kutoka asilimia 30 hadi asilimia 32.5.
Kulingana na sheria hiyo mpya, Wakenya walio na mishahara ya jumla ya kila mwezi zaidi ya dola 5,727 wanapaswa kulipa ushuru mpya wa mapato wa asilimia 35.
Sheria pia ilipandisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotozwa kwa bidhaa za petroli kutoka asilimia 8 hadi 16.
Omtatah amepinga ushuru huo mpya mahakamani akisema unawalemea Wakenya ambao tayari wanabeba mzigo wa gharama ya juu ya maisha.
"Kuwalazimisha wafanyakazi kuchangia kiasi cha pesa kulingana na asilimia inayotumika ya kukatwa bila kuzingatia majukumu yao ya kimkataba yaliyopo juu ya mishahara yao sio jambo la busara," Omtatah alisema katika ombi lake.
Aidha aliteta kuwa seneti ya Kenya haikuhusika katika mchakato wa kutunga sheria, ambao, kulingana naye, ni sawa na ukiukaji wa katiba, kwani Mswada wa Fedha unagusa shughuli za kaunti.
Jaji Mugure Thande aliidhinisha ombi la Omtatah kuwa la dharura, na kusimamisha utekelezaji wa sheria hiyo mpya hadi kesi ya mbunge huyo isikilizwe na kuamuliwa.
Haya yanajiri huku Mamlaka wa Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) ikijiandaa kubadilisha bei ya mafuta siku ya Ijumaa baada ya Mswada wa Fedha wa 2023 kutiwa saini na kuwa sheria.