Jeshi la Polisi la Haiti limefanya operesheni kadhaa dhidi ya makundi ya wahalifu, lakini bado ina changamoto / Picha: AP

Mahakama Kuu imetoa maagizo ya kuzuia serikali kwa muda kupeleka Polisi wa Kenya nchini Haiti.

Hii inafuata ombi lililowasilishwa na kikundi cha Thirdway Alliance ambayo ilidai haikuidhinishwa na Bunge.

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema kuwa katiba inaruhusu Rais William Ruto kupeleka maafisa hao 1000 nchini Haiti kwa idhini ya Bunge.

"Kifungu cha 240 cha katiba kinamtaka rais kupeleka vikosi vyovyote nje ya nchi iwe ni jeshi la taifa au kikosi kingine chochote ambacho kinajumuisha vyombo vya usalama wa taifa, na bunge lazima liidhinishe," Kindiki alisema.

Kutuma vikosi nchini Haiti kumezua mjadala mkubwa hasa nchini Kenya, huku wananchi wengi katika mitandao ya kijamii wakidai kuwa ni wazo baya, kwani Haiti ni mbali na Kenya na pia maafisa hao wa polisi huenda hawataelewa mazingira wanapotumwa.

Tayari baraza la amani na usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa limeidhinisha usaidizi wa Usalama wa Kimataifa unaoongozwa na Kenya nchini Haiti.

Baraza hili lilidai kwamba "watu wa Haiti hatimaye watapata haki".

Uamuzi huu ulikuwa umeungwa mkono na Rais William Ruto ambaye alisema kuwa "haki hatimaye inakuja kwa watu wa Haiti."

Kenya na Marekani Mwezi Septemba mwaka huu zilitia saini mfumo muhimu wa ushirikiano wa kiulinzi.

Mkataba huo muhimu unasisitiza ushirikiano wa kijeshi, unaimarisha ushirikiano wao katika mapambano dhidi ya makundi yenye itikadi kali kama vile al-Shabaab, na kufungua milango kwa Kenya kuongoza ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama nchini Haiti kwa msaada mkubwa wa Marekani.

Mahakama kuu imesema itatoa maagizo zaidi tarehe 24 Oktoba.

Hali ya usalama nchini Haiti

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry aliomba mara ya kwanza kupelekwa kwa kikosi cha kijeshi mwezi Oktoba 2022.

Wakati huo, umoja wa makundi yenye nguvu ya wahalifu uitwao "G9 and Family" ukiongozwa na afisa wa zamani wa polisi ulichukua udhibiti wa kituo muhimu cha mafuta katika mji mkuu wa Port-au-Prince, na kuizorotesha nchi na kufunga upatikanaji wa maji, mafuta, na bidhaa za msingi.

Baadaye, kundi hilo la wahalifu liliruhusu malori ya mafuta kuingia eneo hilo, lakini tangu wakati huo, makundi ya wahalifu yamekuwa yenye nguvu zaidi.

Kuanzia tarehe 1 Januari hadi Agosti 15, zaidi ya watu 2,400 nchini Haiti wameripotiwa kuuawa, zaidi ya 950 kutekwa nyara, na zaidi ya 900 kujeruhiwa, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya watu 200,000 wamepoteza makazi yao wakati makundi ya wahalifu yanapopora jamii wakipigana kwa ajili ya eneo.

Jeshi la Polisi la Haiti limefanya operesheni kadhaa dhidi ya makundi ya wahalifu, lakini chombo hicho cha polisi kina rasilimali finyu, na idadi yake ni ndogo, ikiwa na maafisa 10,000 pekee kwa nchi yenye watu zaidi ya milioni 11.

TRT Afrika